NYAMAGANA, MWANZA
Mhandisi Kwilasa Deogratias Ntare amejiunga na mchakato wa kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Nyamagana kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya kuchukua na kurejesha rasmi fomu ya kuomba kuteuliwa na chama hicho.
Akizungumza mara baada ya kurejesha fomu, Mhandisi Ntare alisema kuwa uamuzi wake umetokana na nia ya dhati ya kuwatumikia wananchi wa Nyamagana na kuendeleza juhudi za maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu, ajira kwa vijana na huduma za kijamii.
“Nimeguswa na changamoto zinazowakabili wananchi wa Nyamagana, na kwa uzoefu wangu kama mhandisi, naamini ninaweza kuchangia katika kuleta suluhisho la kudumu kupitia jukwaa la Bunge,” alisema.
Mchakato wa uchukuaji na urejeshaji fomu za kuomba kuteuliwa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kupitia CCM umeendelea kushika kasi katika maeneo mbalimbali nchini, huku makada na wanachama wa chama hicho wakijitokeza kuonesha nia ya kuwania nafasi za udiwani na ubunge kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.
Kwa sasa, jina la Mhandisi Ntare linasubiri kupitiwa na vikao husika vya chama ili kupata uteuzi wa mwisho wa kugombea ubunge katika jimbo hilo lenye ushindani mkubwa mkoani Mwanza.