Na Philipo Hassan – Hifadhi ya Taifa Mikumi
Kamishna wa Uhifadhi Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), CPA (T) Musa Nassoro Kuji, amewaelekeza Maafisa na Askari Uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa Mikumi kuimarisha utendaji kazi na kuwajibika ipasavyo ili kuimarisha ulinzi wa maliasili zilizopo ndani ya hifadhi kwa ajili ya manufaa kwa kizazi kilichopo na kizazi kijacho.
Kamishna Kuji ameyasema hayo leo Juni 30, 2025, wakati wa kikao kazi na Maafisa na Askari hao, kilichofanyika katika ofisi za Makao Makuu ya Hifadhi yaliyopo eneo la Kikoboga, Mikumi.
Akizungumza katika kikao hicho, Kamishna Kuji alisema “Imarisheni utendaji kazi wenu, ushirikiano, maarifa, uwajibikaji, nidhamu, utii pamoja na ubunifu ili muweze kufanya kazi vizuri na kufikia malengo ya Shirika na Taifa kwa ujumla hasa katika kulinda maliasili hizi kwa faida ya kizazi hiki na kijacho.”
Sambamba na maelekezo ya kiutendaji, Kamishna Kuji aliwahakikishia watumishi wa Hifadhi ya Taifa Mikumi kuwa Shirika linaendelea kuchukua hatua za kuboresha maslahi kwa wafanyakazi ambapo ni pamoja na uboreshaji wa mazingira ya kazi, huduma za afya, motisha mbalimbali kwa Maafisa na Askari ili kuwajengea mazingira bora ya kiutendaji na kuboresha ustawi wa maisha yao.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, John Nyamhanga ambaye ni Mkuu wa Kanda ya Mashariki, alieleza mikakati mbalimbali ya kuboresha ulinzi wa maliasili zilizopo ndani ya hifadhi hiyo pamoja na kukuza utalii.
“Ulinzi umeimarishwa kwa kuhakikisha doria zinafanyika ndani na pembezoni mwa Hifadhi, ambapo kazi hizo zinahusisha udhibiti wa wanyama wakali na waharibifu, doria za mara kwa mara, pamoja na kushirikisha jamii katika uhifadhi,” alieleza Kamishna Nyamhanga.
Aidha, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Augustine Massesa ambaye ni Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mikumi, alimkaribisha Kamishna Kuji na kuwasilisha taarifa ya utendaji kazi. Kamishna Massesa alieleza kuwa idadi ya watalii imeendelea kuongezeka sanjari na mapato yatokanayo na shughuli za utalii.
“Idadi ya watalii imeendelea kuongezeka ambapo kwa kipindi cha Julai 2024 hadi Juni 29, 2025, hifadhi imepokea jumla ya watalii 174,433, sawa na ongezeko la 11.74% ikilinganishwa na matarajio ya watalii 156,100. Idadi hii ni sawa na ongezeko la 25.63% tukilinganisha na idadi ya watalii waliotembelea hifadhi kwa mwaka 2023/2024 ambapo walikuwa 138,844,” aliongeza Kamishna Massesa.
Naye, Askari Uhifadhi Mkuu Okoth Mubaso alimshukuru Kamishana Kuji kwa kufanya ziara katika hifadhi hiyo na kuzungumza na wafanyakazi.
“Tunakushukuru sana Afande kwa kuja kutuona, tunakuahidi tutaendelea kuchapa kazi kwa weledi, nidhamu na kufuata maelekezo ya viongozi wetu ili kuimarisha uhifadhi wa maliasili na kuboresha shughuli za utalii ambazo ni chanzo cha mapato kwa Shirika na Serikali” alisema Mubaso.
Hifadhi ya Taifa Mikumi ni miongoni mwa Hifadhi 21 zinazosimamiwa na TANAPA. Hifadhi hii hifikika kwa urahisi ukitokea Morogoro mjini, na pia imeendelea kuvutia watalii wengi kutokea mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Pwani kutokana usafiri wa Treni ya mwendokasi (SGR).