Na Silivia Amandius
Missenyi, Kagera.
Mvuto wa kisiasa wa kijana mchumi na mkulima Evance Kamenge umeendelea kuonekana wazi baada ya kundi la wanachama 67 kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Wilayani Missenyi, kutangaza kujiunga rasmi na Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakimpongeza Kamenge kwa hatua ya kuchukua fomu ya kuwania ubunge katika jimbo hilo.
Katika hafla fupi iliyofanyika leo Juni 29, 2025, Katibu wa CCM Wilaya ya Missenyi, Bakari Mwacha, aliwapokea rasmi wanachama hao akithibitisha kuwa 22 kati yao tayari wamesajiliwa kupitia mfumo wa kielektroniki wa chama hicho, huku akiahidi kuendelea na mchakato wa usajili kwa wanachama waliobaki hadi watakapokamilika wote.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Remigius Daniel Kamzola ambaye alikuwa Katibu wa CHADEMA kata ya Mabale, alieleza kuwa maamuzi yao yamechochewa na matumaini makubwa waliyonayo kwa uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sambamba na imani waliyonayo kwa Evance Kamenge ambaye wanamwelezea kama kijana jasiri, mzalendo, na mwenye dira ya maendeleo kwa wananchi wa Missenyi.
Wengine walioungana na Kamzola ni pamoja na Apolinary Joseph Kaijage na Halima John ambao wote waliwahi kuwa wanachama wa CHADEMA katika maeneo tofauti ya Missenyi. Kwa pamoja, wameonyesha matumaini makubwa kuwa Kamenge atakuwa chachu ya mageuzi ya kiuchumi na kijamii endapo atapewa ridhaa ya kuwa mbunge.
Hatua hii imezidi kuashiria namna ambavyo jina la Evance Kamenge linavyozidi kushika kasi na kuhamasisha mageuzi ya kisiasa ndani ya jimbo hilo, huku akitazamwa na wengi kama chaguo jipya la matumaini kwa Missenyi.