Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amempokea Rais wa Jamhuri ya Burundi Mheshimiwa Evariste Ndayishimiye aliyewasili nchini kwa ajili ya kushiriki uzinduzi wa Kiwanda cha mbolea cha Itra-Com kilichopo eneo la Nala jijini Dodoma.
Mheshimiwa Ndayishimiye ambaye ameambatana na mwenza wake Mhe. Mama Angeline Ndayishimiye pamoja na Viongozi waandamizi kutoka Serikali ya Burundi aliwasili katika Uwanja wa Ndege wa jijini Dodoma na kulakiwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na baadaye kuelekea Nala ambako yeye na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan watashiriki uzinduzi wa Kiwanda hicho ambacho mwekezaji ni raia kutoka Burundi.