Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa taarifa ya utekelezaji wa ahadi alizozitoa kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wananchi, akieleza mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizojitokeza, na jinsi ustawi wa wananchi ulivyoimarishwa kupitia sera, mipango na miradi ya Serikali tangu mwaka 2021.
Akihutubia na kuhitimisha rasmi shughuli za Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma, Rais Dkt. Samia amesema kipindi cha tangu mwaka 2021 hadi sasa kimekuwa cha kufanya mageuzi makubwa, kuongeza tija katika shughuli za kiuchumi, na kujenga msingi imara wa ukuaji endelevu wenye kasi zaidi na unaowainua wananchi kiuchumi. Aidha, kimekuwa kipindi cha kuimarisha ustahimilivu wa jamii, kukuza ustawi wa wananchi na kuwawezesha ili kujiletea maendeleo.
Halikadhalika, ameeleza kuwa uchumi umekua kutoka wastani wa asilimia 3.9 mwaka 2021 hadi asilimia 5.5 mwaka 2024 na unatarajiwa kufikia asilimia 6 mwaka 2025. Miongoni mwa mafanikio ya kisekta aliyoyataja ni kuanza kwa treni ya mizigo ya SGR, kukamilika kwa ujenzi wa Daraja la John Pombe Magufuli, uboreshaji wa viwanja vya ndege, na ujenzi wa meli mpya kwa ajili ya usafiri wa majini.
Kuhusu Deni la Taifa, Rais Dkt. Samia amesema ongezeko lake limechangiwa na kuiva kwa madeni ya nyuma, kupanda kwa riba kimataifa, tofauti za viwango vya ubadilishaji fedha na uamuzi wa Serikali kutambua madeni ya kabla ya mwaka 1999 ya mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuilinda na kuwezesha wastaafu kulipwa pensheni.
Vilevile, Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa licha ya kupungua kwa baadhi ya misaada ya kimataifa, Serikali itahakikisha shughuli za kijamii, hasa katika sekta ya afya ikiwemo mapambano dhidi ya UKIMWI, haziathiriki, na kusisitiza kuwa afya za Watanzania zitaendelea kuwa kipaumbele cha Serikali.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amempongeza Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson kwa uongozi wake mahiri uliowezesha kufanyika kwa mikutano 19 ya Bunge hilo na kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa 31 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU). Vilevile, amewashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa ushirikiano wao kwa Serikali katika kipindi chote cha uongozi wake.
Rais Dkt. Samia ametoa wito kwa Watanzania kuendeleza amani na mshikamano wakati wote hususan katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, akisisitiza kuwa amani na utulivu ndio msingi wa mafanikio ya pamoja kama Taifa.
Rais Dkt. Samia pia ameeleza kuwa maridhiano na mashauriano ya kisiasa yamechochea mageuzi makubwa yakiwemo urejeshaji wa mikutano ya hadhara, kuanzishwa kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, kufutwa kwa utaratibu wa mgombea kupita bila kupingwa, na utoaji wa ruzuku kwa vyama vya siasa vinavyostahili.
Aidha, Rais Dkt. Samia amesema kuwa Serikali itaendelea kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Maridhiano, ikiwemo kuanza upya kwa mchakato wa Katiba Mpya katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Vilevile, Rais Dkt. Samia ametoa rai kwa vyama vya siasa kuwateua wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuwania nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Rais Dkt. Samia amehitimisha shughuli za Bunge la 12 na kutangaza kuwa Bunge litavunjwa rasmi tarehe 03 Agosti 2025, hatua inayowezesha kuanza kwa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2025.