Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Asia Abdallah, Juni 28, 2025, amejitokeza kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu hiyo, Asia Abdallah amesema amehamasika kuwania nafasi hiyo kwa lengo la kuwaletea wanawake wa Mkoa wa Dodoma maendeleo endelevu, huku akisisitiza kuwa muda umefika kwa wanawake kuwa mstari wa mbele katika uongozi na ustawi wa jamii.
Kauli mbiu yake katika kinyang’anyiro hicho ni “Tumaini Jipya la Wanawake Mkoa wa Dodoma”, ikiwa ni wito wa matumaini mapya, usawa wa kijinsia, na ustawi wa wanawake kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Asia Abdallah ni miongoni mwa viongozi waliowahi kushika nyadhifa mbalimbali za kiutendaji serikalini, huku akihusisha uzoefu wake wa uongozi na maono mapya katika kuwatumikia wananchi.
Zoezi la uchukuaji wa fomu za kugombea nafasi mbalimbali ndani ya CCM limeanza Juni 28, 2025 na linaendelea katika mikoa yote nchini, huku wagombea mbalimbali wakiendelea kujitokeza kueleza dhamira zao za kugombea uongozi ndani ya chama hicho.