Dar es Salaam
Imeelezwa kwamba uwepo wa mvua nyingi jijijini Dar es Salaam imepelekea ujenzi wa barabara katika maeneo yenye zabuni kusimama kufanya kazi katika kipindi cha miezi miwili.
Hayo yameelezwa na Meneja wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Geofrey Mkinga wakati akikagua maeneo ambayo yapo chini ya wazabuni.
Akikagua barabara ya Tabata-Mazda (mita 500), Tabata-Kinyerezi kuelekea Sokoni (kiwango cha zege) pamoja na barabara ya Kivule-Msongola (km 9) na barabara kuelekea hospitali ya wilaya na Majohe (Km. 2.7).
“Kama tulivyotoa taarifa mwanzo kwamba kazi nyingi zilikuwa zimesimama kutokana na uwepo wa mvua nyingi zilizonyesha hivyo kwasasa tumeshawaagiza wakandarasi warudi ‘site’ na kuanza kazi mara moja”.
“Wakati wa mvua nyingi wakandarasi hawakuweza kukusanya malighafi na hata kuingia kwenye machimbo, pia huwezi kuweka ‘material’ ya udongo kipindi hicho’ aliongeza kusema.
Hata hivyo, Mhandisi huyo aliwataka wakandarasi wote waliopewa zabuni za ujenzi wa barabara katika mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha wanaingia kazini ili kazi walizopewa zikamilike kwa wakati.
Kwa barabara ya Msongola-Kivule, Mhandisi Mkinga amemuagiza Mkandarasi kuendelea na kazi hiyo hadi Desemba mwaka huu awe ameshatoka hatua za awali na kubakiza kuweka tabata la lami pamoja na mifereji.
“Kama unavyoona kuelekea hospitali ya wilaya na Majohe, ilikuwa barabara mbovu na wananchi wamekuwa wakilalamikia ila kwa sasa hamna kazi iliyosimama na maendeleo ya mradi ni mazuri.
Naye, Meneja wa Ilala Mhandisi John Magori amesema wataendelea kuwabana wakandarasi kuhakikisha maeneo yote yenye mikataba yanafanyiwa kazi kwa wakati ili kusudi changamoto za barabara ziishe.
Amesema, wakandarasi katika kata zote wameshaanza kurudi ‘site’ na kazi zimeanza ikiwemo katikati ya jiji, Tabata, Kitunda na Upanga.
Mkazi wa Msongola, Bw. Peter Marwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa barabara hizo kwani itawaondolea adha ya usafiri katika Kata ya Msongola-Jimbo la Kivule.
Wakati huo huo, Mkandarasi anayejenga barabara ya Segerea, Mhandisi Lookman Msanguka amesema kazi zilisimama kwa kipindi fulani ila kwa sasa kazi zinaendelea na hivyo ameaahidi kufanya kazi na kukamilisha mradi huo kama ulivyopangwa.
“Changamoto zilikuwepo kutokana na mvua kwani huwezi kufanya kazi ya zege na kushindilia vifusi kipindi cha mvua hivyo tulisimama kwa miezi miwili ila kwasasa tunapambana ili kwenda sawa na kilichokuwepo kwenye mikataba”.