Mwenyekiti wa Mfuko wa Fursa sawa kwa wote EOTF Mama Anna Mkapa (wa pili kutoka kushoto waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wanawake wajasiriamali kati ya wanawake 250 nchi nzima wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyofanyika jijini Dar es salaam. Kulia kwa Mama Mkapa ni Mgeni rasmi Bi. Gema Akilimali.
………………..
Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Imebainika kuwa kadri kasi ya mabadiliko duniani inavyozidi kuongezeka, suala la kuwawezesha wanawake kiuchumi limeendelea kushika nafasi ya juu katika ajenda za maendeleo duniani.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Bi. Gema Akilimali ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mafunzo kwa wanawake wajasiriamali 250 kutoka mikoa mbalimbali nchini. Mafunzo hayo yaliandaliwa na Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF) chini ya kaulimbiu isemayo “Mwanamke ni Nguvu Imara ya Asili ya Jamii.”
Akizungumza katika hafla hiyo, Bi. Akilimali alisema kuwa mafanikio ya maendeleo ya jamii yoyote hayawezi kufikiwa pasipo kushirikisha kikamilifu wanawake, hasa katika masuala ya kiuchumi.
“Wanawake ni msingi wa familia na jamii. Kuwajengea uwezo kiuchumi ni kuwekeza katika ustawi wa kizazi cha sasa na kijacho,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa EOTF Mama Anna Mkapa alisema taasisi hiyo isiyo ya kiserikali ilianzishwa mwaka 1997 kwa lengo la kuwawezesha wanawake wa Tanzania kupambana na changamoto za umasikini, ujinga na maradhi.
Mama Mkapa aliwataka wanawake kutumia fursa ya mafunzo hayo kama chachu ya kuimarisha shughuli zao za kiuchumi na kuchangia katika maendeleo ya taifa kwa ujumla.
“Tunaamini mwanamke akiwa imara, familia na jamii pia zitakuwa imara. Hivyo, uwezeshaji huu ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma kimaendeleo,” alisisitiza Mama Mkapa.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwapa washiriki ujuzi na mbinu za kuboresha biashara, kukuza mitaji na kuongeza tija katika shughuli zao za kiuchumi.