Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya CDF CUP 2025, Brigedia Jenerali Saidi Hamis Saidi akizungumza na waandishi wa habari leo, Juni 23, 2025, jijini Dar es Salaam kuhusu Mashindano ya Mkuu wa Majeshi (CDF CUP 2025) yatakayofanyika kuanzia Julai 2 hadi 14, 2025, Dar es Salaam. (PICHA NA NOEL RUKANUGA)
Mkurugenzi wa Utimamu wa Mwili, Michezo, Sanaa na Utamaduni wa JWTZ, Kanali David Luoga akizungumza na waandishi wa habari leo, Juni 23, 2025, jijini Dar es Salaam kuhusu Mashindano ya Mkuu wa Majeshi (CDF CUP 2025).
Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Utafiti kutoka SUMAJKT, Kanali George Wang’ombe akizungumza na waandishi wa habari leo, Juni 23, 2025, jijini Dar es Salaam kuhusu Mashindano ya Mkuu wa Majeshi (CDF CUP 2025).
Msemaji Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Kanali Gaudentius Ilonda akizungumza na waandishi wa habari leo, Juni 23, 2025, jijini Dar es Salaam kuhusu Mashindano ya Mkuu wa Majeshi (CDF CUP 2025).
Picha za matukio mbalimbali.
………………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Stergomena Tax, anatarajiwa kufungua rasmi Mashindano ya Mkuu wa Majeshi (CDF CUP 2025) yatakayofanyika kuanzia Julai 2 hadi 14, 2025 jijini Dar es Salaam, mashindano ambayo yamebeba kaulimbiu isemayo “Michezo ni Umoja na Mshikamano.”
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Juni 23, 2025, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya CDF CUP 2025, Brigedia Jenerali Saidi Hamis Saidi, amesema kuwa mgeni rasmi katika sherehe za ufungaji anatarajiwa kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Jacob Mkunda.
Brigedia Jenerali Saidi amesema mashindano hayo yana lengo la kuwakutanisha wanajeshi kutoka vikosi vyote vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wakiwemo Maafisa, Askari, na watumishi wa umma.
“Michezo ni sehemu ya majukumu ya kila siku ya wanajeshi. Kupitia mashindano haya, wanajeshi huimarisha utimamu wa mwili, afya ya akili, moyo wa kishujaa, ujasiri, ukakamavu, kujiamini, na pia kubaini na kukuza vipaji vya michezo. Pia yanaimarisha mahusiano kati ya Jeshi na jamii,” amesema Brigedia Jenerali Saidi.
Aidha, ameongeza kuwa mashindano haya yatachochea mshikamano, upendo, undugu na uzalendo miongoni mwa wanajeshi na raia, ambapo timu kutoka kamandi zote zitashiriki, zikiwemo Kamandi ya Jeshi la nchi kavu, Jeshi la Anga, Jeshi la Wanamaji, Jeshi la Akiba, Makao Makuu ya Jeshi, na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Brigedia Jenerali Saidi amefafanua kuwa mwaka huu mashindano yatakuwa na mvuto zaidi kutokana na kuongezwa kwa michezo mipya yenye asili ya kijeshi pamoja na michezo ya kimashindano.
Amesema kuwa michezo ya kimashindano itakayoshindaniwa ni mpira wa miguu kwa wanaume, mpira wa netball kwa wanawake.
Michezo mengine watakaoshiriki wanaume na wanawake ni pamoja na mpira wa mikono, mpira wa kikapu, mpira wa wavu, riadha, ngumi, mieleka, kuruka vikwazo, kuogelea, vishale, golfu na shabaha.
Mashindano hayo yatatumia viwanja mbalimbali kulingana na aina ya mchezo. Uwanja wa Azam Complex utatumika kwa mechi ya mpira wa miguu siku ya ufunguzi na ufungaji.
Viwanja vya Kambi ya Generali Twalipo – Mgulani vitatumika kwa michezo ya mpira wa kikapu, netiboli, mikono, wavu, ngumi, mieleka na kuruka viunzi.
Viwanja vya Lugalo Golf Club vitatumika kwa mchezo wa golfu, huku fukwe za Msasani zikitumika kwa mchezo wa vishale.
Viwanja vya 501 Lugalo vitatumika kwa mechi za mpira wa miguu, na michezo ya kuogelea itafanyika Makao Makuu ya Kamandi ya Wanamaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utimamu wa Mwili, Michezo, Sanaa na Utamaduni wa JWTZ, Kanali David Luoga, amesema kuwa mwaka jana mshindi wa jumla alikuwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), hivyo mwaka huu mashindano yanatarajiwa kuwa na ushindani mkali zaidi.
Naye Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Utafiti kutoka SUMAJKT, Kanali George Wang’ombe, amesisisitiza kuwa SUMAJKT wanatambua na kuthamini nafasi ya michezo na utamaduni katika kukuza uzalendo, kwani ni sehemu muhimu ya Jeshi la Kujenga Taifa.
Mashindano haya ya CDF CUP 2025 yameratibiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).