Na Emmanuel J. Shilatu
Tangu aapishwe kuwa Rais wa Awamu ya sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameonyesha sura kuu 3 ambazo zinampa kicheko na matumaini makubwa ya ushindi kwenye uchaguzi Mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais mnamo mwezi Oktoba 2025.
A: UHODARI NA TUMAINI
Rais Samia amepokea kijiti cha Urais kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa 5 wa Tanzania Hayati Dkt John Magufuli na wa kipindi chote ameliongoza vyema Taifa kwa uhodari wa ufariji kwa Watanzania wote. Rais Samia amewafariji wafiwa upande wa familia, amewafariji Watanzania na kujawa faraja, tumaini na nguvu mpya.
Rais Samia ameonyesha uhodari katika ulezi ambapo amesimama kama Mama ndani ya uongozi kwa kuwapa onyo, angalizo ambalo ni sawa na kuwapa fursa nyingine ya kujisahihisha ili safari ijayo vijana wakizingua basi Mama atawazingua vyema.
Rais Samia ameonyesha namna alivyo komaa kiuongozi kwa kusimamia vyema utawala wa sheria kwa kuwasimamisha wenye tuhuma kwanza kupisha uchunguzi na sio kuwatimua moja kwa moja pasipo kutoa nafasi ya kumsikiliza ili kubaini ukweli wa tuhuma.
Huyo ndio Mama yetu Rais Samia. Rais Samia aliyeanza kwa kutoa maagizo vyombo vya habari vilivyofungiwa vifunguliwe. Nyota njema ya uendelezwaji wa uhuru wa habari nchini uliokuwapo miaka na miaka.
B: UZALENDO
Rais Samia ameonyesha uzalendo wa kuzilinda rasilimali zetu nchini kama ambavyo mtangulizi wake Hayati Dkt Magufuli amefanya. Mathalani, Rais Samia amekemea utoroshwaji na uchimbaji kiholela wa madini ya Tanzanite kwenye machimbo ya mererani.
Ni Rais Samia huyu huyu kwa kipindi Cha Urais wake ameboresha Sheria ya Madini ambayo imezaa matunda kwa Watanzania ndani ya kipindi Cha muda mfupi tu.
C: UCHAPA KAZI
Katika kuonyesha zege halilali, Rais Samia ndani ya muda mfupi ameendeleza urithi wa miradi ya kimkakati ya kimaendeleo aliyoiacha Hayati Dkt Magufuli. Sote ni mashuhuda Reli ya SGR inasafiri kwa Kasi kusafirisha abiria na mizigo; Umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere umeingiza megawatts 2115 kwenye gridi ya Taifa, Daraja la Kigongo – Busisi na Madaraja mengineyo yameanza kutumika n.k
Pia amesimamia kwa vitendo kupambana usiku na mchana kuhakikisha ilani ya uchaguzi 2020 – 2025 inatekelezwa kwa vitendo na kukamilika. Hapo alikuwa na viporo vya miradi mikubwa ya Matrilioni ya fedha ya kimkakati iliyoachwa na Mtangulizi wake Hayati Dk Magufuli lakini bado akaweza kutekeleza ilani ya uchaguzi, si kazi rahisi na nyepesi kama tudhaniavyo
Itoshe kusema kazi inaendelea kupitia sura 3 za uchapa kazi, uzalendo na uhodari wa Rais Samia utampa kicheko Cha ushindi wa kishindo Dk. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi Cha miaka Mitano mingine na nyota yake utaipa kicheko Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Ndugu zangu, Tuendelee kunywa mtori, nyama tumezikaribia.
Shilatu, E.J