::::::::
Na Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam
Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICTC) kwa kushirikiana na Mtandao wa Vituo vya Ubunifu Tanzania (Tanzania Hubs Network – THN) wamesaini makubaliano ya ushirikiano wa kimkakati kwa lengo la kuimarisha uwezo wa vituo vya ubunifu nchini katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Makubaliano hayo yaliyofikiwa jijini Dar es Salaam yameelezwa kuwa ni hatua mpya katika kuimarisha uratibu wa ukuaji na matumizi ya TEHAMA nchini, hasa katika kuchochea ubunifu miongoni mwa vijana na wajasiriamali.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kusainiwa kwa makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dk. Nkundwe Mwasaga alisema ushirikiano huo utaisaidia Tume kuwa karibu zaidi na vituo vya ubunifu nchini kote, hali itakayorahisisha kutambua na kuendeleza bunifu mbalimbali zinazochangia kwenye uchumi wa kidijitali.
“Hii ni hatua muhimu kwa Tume ya TEHAMA. Ushirikiano huu utasaidia kuhamasisha maendeleo ya TEHAMA kupitia bunifu mbalimbali zinazotoka kwenye vituo hivi, ambavyo mara nyingi vinabeba mawazo na suluhisho ya changamoto zinazowakabili Watanzania,” alisema Dk. Mwasaga.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Mtendaji wa THN, Kiko Kiwanga alisema kuwa makubaliano hayo yatafungua milango ya ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na vituo vya ubunifu, hatua itakayosaidia kubaini na kutatua changamoto zinazokwamisha vijana na wajasiriamali nchini kutumia TEHAMA kuibua fursa za kiuchumi.
“Makubaliano haya ni jukwaa la pamoja kati yetu na Serikali, si tu kwa ajili ya kuboresha mazingira ya ubunifu, bali pia kusaidia vijana kufanikisha mawazo yao ya kiteknolojia na kuyageuza kuwa miradi yenye tija,” alisema Kiwanga.
Makubaliano hayo yamekuja wakati ambapo Serikali inaendelea kusisitiza umuhimu wa TEHAMA kama nyenzo muhimu katika kuharakisha maendeleo ya uchumi wa kidijitali na kuongeza ushindani wa taifa katika soko la kimataifa.
——