Naibu Katibu Mkuu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Daniel Mushi (kushoto) akimkabidhi zawadi Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa katika hafla ya ufunguzi wa Kongamano la 13 la Kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) lililofanyika leo Juni 18, 2025 katika Ukumbi wa Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika Mashariki, Kampasi ya Mloganzila, Dar es Salaam (PICHA NA NOEL RUKANUGA)
Makamu Mkuu wa Chuo MUHAS Prof. Appolinary Kamuhabwa akizungumza na waandishi wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 13 la Kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) lililofanyika leo Juni 18, 2025 katika Ukumbi wa Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika Mashariki, Kampasi ya Mloganzila, Dar es Salaam.
Naibu Mkuu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Daniel Mushi akizungumza na waandishi wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 13 la Kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) lililofanyika leo Juni 18, 2025 katika Ukumbi wa Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika Mashariki, Kampasi ya Mloganzila, Dar es Salaam.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza wakati akifungua Kongamano la 13 la Kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) lililofanyika leo Juni 18, 2025 katika Ukumbi wa Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika Mashariki, Kampasi ya Mloganzila, Dar es Salaam.
Kaimu Naibu Makamu wa Mkuu wa Chuo MUHAS, Idara ya Tafiti na Ushauri wa Kiutaalamu Prof. Bruno Sunguya akizungumza na waandishi wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 13 la Kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) lililofanyika leo Juni 18, 2025 katika Ukumbi wa Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika Mashariki, Kampasi ya Mloganzila, Dar es Salaam.
………………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amewataka watafiti nchini kuwekeza katika tafiti zenye tija na kuhakikisha matokeo ya tafiti hizo yanawasilishwa kwa watunga sera ili yaweze kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Akizungumza leo, Juni 18, 2025, jijini Dar es Salaam wakati akifungua Kongamano la 13 la Kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), lililofanyika katika Ukumbi wa Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika Mashariki, Kampasi ya Mloganzila.
Katika hotuba yake, Mhe. Majaliwa amesema kuwa kupitia machapisho ya kisayansi, watafiti wana nafasi ya kuishauri Serikali na wadau kuhusu njia bora za kuongeza ushiriki wa wananchi katika mapambano dhidi ya magonjwa na kupambana na taarifa potofu zinazoenea kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii.
Aidha, amesisitiza kuwa sasa ni wakati muafaka kwa watafiti na watunga sera kushirikiana kwa karibu ili kufanikisha tafiti zinazobaini mahitaji halisi ya jamii, zenye uwezo wa kuchochea uzalishaji wa ndani, na hivyo kuchangia maendeleo ya kitaifa.
“Tunaipongeza MUHAS kwa maendeleo makubwa ya miradi ya kimkakati inayoendelea, ikiwemo ujenzi wa kampasi mpya Kigoma na Mloganzila, pamoja na awamu ya pili ya mradi wa Kituo cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa. Maendeleo haya ni kielelezo cha jitihada za Serikali katika kupambana na magonjwa yasiyoambukiza na kuboresha mifumo ya afya nchini,” amesema Mhe. Majaliwa.
Ameongeza kuwa kongamano hilo liwe jukwaa la kuangazia mafunzo, huduma, sera, na miongozo ya teknolojia katika sekta ya afya, huku akisisitiza umuhimu wa sekta binafsi na ya umma kushirikiana kwa lengo la kuongeza ufanisi na uzoefu wa pamoja.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, ambaye alimwakilisha Waziri wa Wizara hiyo, amesema kuwa uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali umetokana na matokeo chanya yanayoonyeshwa na MUHAS katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.
“Katika miaka ya hivi karibuni, chuo hiki kimefanikiwa kuingia miongoni mwa vyuo vitano bora katika Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, jambo linalothibitisha ubora wa mafunzo, tafiti zenye tija, na weledi wa hali ya juu wa wakufunzi wake,” amesema Prof. Mushi.
Ameeleza kuwa tafiti zinazofanywa na MUHAS zimechangia kwa kiwango kikubwa katika kuandaa na kuimarisha sera, miongozo, na mipango mbalimbali katika sekta ya afya na elimu.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Prof. Appolinary Kamuhabwa, ameishukuru Serikali kwa usaidizi mkubwa uliowezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo inaleta mageuzi katika mazingira ya elimu ya juu na huduma za afya nchini.
Prof. Kamuhabwa ameeleza kuwa kaulimbiu ya kongamano hilo ni: “Kubadili Mifumo ya Afya Afrika: Kuweka Kipaumbele katika Bunifu na Tafiti katika Kukabiliana na Changamoto Nyumbufu za Afya Duniani.”
Amesema kuwa kaulimbiu hiyo imechaguliwa kwa kutambua umuhimu wa kuimarisha mifumo ya afya kwa kutumia ushahidi wa kisayansi, teknolojia bunifu, na ushirikiano wa sekta mbalimbali ili kukabiliana na changamoto mpya na endelevu kama vile milipuko ya magonjwa, mabadiliko ya tabianchi, na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza.
Kwa mujibu wa Prof. Kamuhabwa, katika kongamano hilo kutakuwa na zaidi ya 200 ya mawasilisho ya tafiti yatakayotolewa kwa njia ya mazungumzo (Oral Presentations) na kwa njia ya mabango (Posters), yakihusisha washiriki kutoka Tanzania na nchi nyingine zikiwemo Kenya, Marekani, Norway, na Zambia. Jumla ya washiriki ni 218.
Amesema kuwa mada zitakazowasilishwa zitahusu ni Magonjwa yasiyoambukiza, Magonjwa ya kuambukiza na usugu wa vimelea, Afya ya mama, mtoto na kijana, Tiba mbadala na tafiti za chanjo, Afya ya kinywa, macho, masikio, pua na koo, Afya ya akili na usalama kazini, Teknolojia na mifumo ya afya jumuishi.
Kuhusu mawasilisho makuu, Prof. Kamuhabwa amesema: Siku ya kwanza, kutakuwa na mada kuu: “Kubadili Mifumo ya Afya Afrika: Kuweka Kipaumbele kwa Bunifu na Tafiti kwa Kukabiliana na Changamoto Zinazobadilika za Afya Duniani,” itakayowasilishwa na Dkt. Nyanda Elias kutoka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).
Siku ya pili, mada kuu itakuwa: “Kukabiliana na Uhalisia wa Magonjwa Mahututi Barani Afrika: Kuweka Kipaumbele kwa Mahitaji Muhimu ya Kujenga Mifumo Thabiti ya Afya,” itakayowasilishwa na Prof. Tim Baker na Dkt. Karima Khalid kutoka MUHAS.
Kongamano hilo litafanyika kwa siku mbili, kuanzia Juni 18 hadi 19, 2025