Na WAF, Djibouti
Waziri wa Afya wa Tanzania Mhe. Jenista Mhagama amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya Mawaziri wa Afya na Masuala ya Afya ya Jamii Kanda ya Mashariki Afrika (The Regional Streering Committee- ResCo).
Mawaziri wa Afya wa kutoka nchi 14 wanachama wa Kanda ya Mashariki mwa Afrika Juni 17, 2025 walipendekeza na kumpitisha Waziri Mhagama kushika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka miwili.
Hatua hii ni mwendelezo wa kutambua uwezo wa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kujenga mahusiano mazuri ya kidiplomasia kimataifa na kikanda.
Wajumbe kwa pamoja walikubaliana Mhe. Waziri Jenista Mhagama katika kupindi kifupi ambacho amekuwa Waziri wa Afya, ameonesha uwezo mkubwa na ushawishi wa kupeleka mbele agenda zinazohusu Afya kwa ushirikiano na mawaziri wenzake kikanda na wanaona kuwepo wake kwenye safu ya uongozi kama makamu mwenyenyiki wa kamati ya Kanda ya Mashariki utaongeza ushawishi kwa nchi wanachama kutoa kipaumbele kwa sekta ya afya na maslahi mapana ya nchi wanachama.
Kamati hiyo tendaji ambayo ipo chini ya Umoja wa Afrika (AU), Mwenyekiti wake ni Waziri wa Afya wa Djibouti, Mhe. Dkt. Ahmed Robleh Abdillah, ina majukumu ya kutoa muongozo wa kimkakati wa afya ya jamii kikanda, kupitia na kupitisha vipaumbele vya kikanda, kuunga mkono uhamasishaji na upatikanaji wa rasilimali pamoja na kupitisha mapendekezo ya kamati ya wataalam kupitia sekretarieti ya Afrika CDC.
Mkutano huo wa Mawaziri wa afya ambao pia Waziri wa Afya wa Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui ameshiriki, ulitanguliwa na mkutano wa wataalam wa Afya ambao ulipendekeza nafasi za wenyeviti na makamu wenyeviti wa Sekretarieti ya wataalam na kamati tendaji ya Mawaziri ambapo Tanzania iliwakilishwa Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe.
Nchi wanachama Kanda ya Mashariki mwa Afrika ni na Tanzania, Kenya, Uganda, Ethiopia Rwanda, Somalia, Sudan ya Kusini, Djibouti, Comoro, Eritrea, Madascar, Mauritania, Seychelles na Sudan.