Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo Kati ya China na Afrika (China-Africa Development Fund) umeahidi kuendelea kuipa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kipaumbele katika kufadhili miradi ya uwekezaji na biashara.
Ahadi hiyo imetolewa wakati Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) alipofanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Mfuko huo, Bw. Wang Shaodan tarehe 17 Juni, 2025, jijini Beijing, China.
Katika mazungumzo hayo Mhe. Waziri Kombo aliishukuru CADFund kwa kufadhili na kuwekeza katika miradi ya uwekezaji na biashara nchini Tanzania. Uwekezaji huo ni katika kutekeleza makubaliano yanayofikiwa kupitia Jukwaa la Ushirikiano la China na Africa (FOCAC). Mhe. Kombo ameutaka Mfuko huo kuongeza zaidi kiwango cha fedha kinachotengwa kwa miradi ya Tanzania.
Awali Mwenyekiti Wang Shaodan alieleza kuwa kufuatia ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na China, tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006, Mfuko huo umeshasaini makubaliano ya kutekeleza miradi yenye thamani ya zaidi ya Dola za Kimarekani millioni 800 nchini Tanzania. Hivi sasa Mfuko huo unawezesha miradi yenye thamani ya Dola za Marekani zaidi ya milioni 73 nchini Tanzania.
Pia, alieleza kuwa mfuko wa CADFund unashika nafasi ya pili kwa ukubwa wa uwekezaji barani Afrika na kwa upande wa Tanzania umewezesha uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo kilimo, uzalishaji wa saruji, utangazaji, teknolojia ya habari na mawasiliano. Hivi sasa Mfuko huo pia upo katika mchakato wa kuwekeza kwenye mradi wa kipaumbele wa uboreshaji wa reli ya TAZARA. Sekta nyingine zinazopewa kipaumbele katika uwezeshaji ni viwanda, ujenzi wa miundombinu na usafirishaji.
Kadhalika, alikiri kuwa ziara ya Waziri Kombo nchini China na kutembelea Mfuko huo ni uthibitisho wa nia ya dhati ya Serikali ya Tanzania ya kutaka kuharakisha uwezeshaji wa utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Kwa upande wake Mheshimiwa Kombo alieleza kuwa ushirikiano baina ya Tanzania na China ni wa kipekee na wa mfano. Hivyo, aliitaka CADFund kutanua wigo wa uwekezaji wake nchini na kuwekeza katika maeneo mengine hususan kilimo cha soya, kuongeza thamani ya madini na utalii ili kuakisi maeneo mapya ya ushirikiano na nchi za Afrika yaliyotangazwa na Serikali ya China katika mkutano wa Waratibu wa Utekelezaji wa Makubaliano ya FOCAC uliofanyika hivi karibuni katika jiji la Changsha, jimbo la Hunan, China.
Kadhalika ilielezwa kwamba Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo Kati ya China na Afrika umekuwa ukifanya kazi na sekta binafsi za Tanzania na China ili kuwezesha uwekezaji na biashara. Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Bw. Wu Guohua, Rais wa Benki ya Maendeleo ya China ambae alieleza kwamba Benki hiyo imetenga takribani Dola za Marekani milioni 60 kwa ajili taasisi za kifedha nchini Tanzania kuwezesha wafanyabiashara wadogo na wa kati (MSMEs).