Na Silivia Amandius.
Bukoba.
Katika mafanikio ya kupongezwa, Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba imevuka lengo la makusanyo ya mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2024/25, ikikusanya Shilingi Bilioni 3.4 hadi kufikia Mei 31, 2025, kutoka lengo la awali la Bilioni 3.1 – sawa na asilimia 112 ya lengo.
Akihutubia kikao maalum cha baraza la madiwani kilichoitishwa Juni 16, 2025 katika ukumbi wa Chemba kwa ajili ya kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Fatma Mwasa aliipongeza halmashauri kwa mafanikio hayo na kwa kupata hati safi katika ukaguzi wa mwaka wa fedha 2023/24.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kuwa halmashauri yako imepata hati safi. Nawapongezeni sana kwa jitihada zenu, ambazo zimechangia kwa kiasi kikubwa kupata matokeo haya chanya,” alisema RC Mwasa mbele ya baraza hilo.
Akiwasihi viongozi na watendaji kuendeleza nidhamu na uwajibikaji, Mhe. Mwasa alisisitiza kuwa mafanikio hayo ni ushahidi wa usimamizi thabiti wa sheria na miongozo ya serikali. Alikumbusha kuwa kupata hati safi si kazi rahisi, lakini kuendelea kuipata kila mwaka kunahitaji kujituma zaidi.
Aliongeza kuwa moja ya vipimo vya utendaji kazi wa halmashauri ni uwezo wake wa kukusanya mapato ya ndani, jambo ambalo Halmashauri ya Bukoba imefanya vizuri kwa mwaka huu wa fedha.
Katika hitimisho la hotuba yake, RC Mwasa alitoa wito kwa halmashauri kuhakikisha inatumia mfumo wa kisasa wa ukusanyaji mapato uitwao TAUSI, huku akisisitiza umuhimu wa kudhibiti ushuru wa mabango na kodi za majengo ili kuongeza mapato zaidi.
Kwa upande wake, Diwani wa Kaibanja Mhe. Jason Rwankomezi, akizungumza kwa niaba ya madiwani, alimshukuru Mkuu wa Mkoa kwa ushirikiano wake na kufika kwenye kikao hicho muhimu. Aliahidi kuwa baraza la madiwani litaendelea kushirikiana kikamilifu na uongozi wa halmashauri katika kuimarisha utendaji na uwajibikaji.