Na John Bukuku, Dar es Salaam
Mabadiliko ya mitaala ya elimu yaliyoanza kutekelezwa mwaka 2023 yameendelea kuzaa matunda, ambapo walimu nchini wameonesha ubunifu na umahiri wa hali ya juu katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na mbinu shirikishi za kisasa katika ufundishaji.
Akizungumza Juni 14, 2025 jijini Dar es Salaam katika hafla ya utoaji wa zawadi kwa washindi wa Shindano la Stadi za Ufundishaji, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba, amesema kuwa mashindano hayo ni jukwaa muhimu linalothibitisha utekelezaji wa mitaala mipya kwa vitendo, hasa kupitia ujumuishaji wa TEHAMA katika masomo ya Sayansi na Hisabati.
“Shindano hili ni njia mojawapo ya kuhakikisha kuwa walimu wetu wanakuwa na uwezo wa kutumia teknolojia na mbinu bunifu kufundisha kwa namna inayowasaidia wanafunzi kupata stadi muhimu za karne ya 21,” alisema Dkt. Komba.
Dkt. Komba aliipongeza Benki ya Dunia kwa kuendelea kufadhili mashindano hayo kupitia miradi ya BOOST na SEQUIP, ambayo inalenga kuboresha uwezo wa walimu kupitia Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini (MEWAKA).
Katika mashindano hayo, walimu kumi kutoka shule za msingi na sekondari walitunukiwa zawadi kutokana na kuonesha umahiri mkubwa katika kufundisha masomo ya Kemia, Fizikia, Baiolojia na Hisabati. Washindi wa kwanza kwa kila somo walijinyakulia Shilingi milioni nne, huku wengine wakipata zawadi mbalimbali kulingana na nafasi zao.
Hafla hiyo imeweka wazi kuwa, pamoja na maboresho ya mitaala, uwezo na ubunifu wa walimu ni kiungo muhimu katika mageuzi ya elimu nchini.