Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma kuongeza kasi ya kushughulikia hoja zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), licha ya halmashauri hiyo kupata hati safi.
Akizungumza katika Baraza Maalum la Kujadili Hoja za CAG kwa Mwaka wa Fedha 2023/24, lililofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Namtumbo, Kanali Ahmed alisisitiza umuhimu wa kuongeza juhudi katika utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa na CAG.
“Nimesikia hapa kulikuwa na hoja 27, kati ya hizo ni 7 tu ndizo zimefanyiwa kazi na kufungwa, 20 zipo kwenye utekelezaji. Hii kasi ya kushughulikia hoja ni ndogo, mnahitajika kuongeza bidii, umakini na uharaka wa utekelezaji,” alisema Kanali Ahmed.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Phiniel Mbula, alibainisha kuwa ofisi ya mkoa inatoa vyeti kwa watumishi waliosaidia upatikanaji wa hati safi.
Alilitaja lengo la kutoa vyeti hivyo ni kutambua mchango wa wafanyakazi, mkurugenzi, madiwani na sekretarieti ya mkoa, ambao wamesimamia vyema taratibu za kifedha, uadilifu na uzalendo.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Namtumbo, Fransis Mgoloka, akimwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo, aliipongeza halmashauri kwa mafanikio yaliyopatikana. Aliahidi kuendelea kufuatilia na kusimamia hoja zilizosalia, ili hatimaye zifungiwe na halmashauri ipate alama ya juu ya uwajibikaji.
Kanali Ahmed alihitimisha kwa kusisitiza kuwa usimamizi wa fedha za umma si lele mama, bali ni wajibu wa kisheria na kimaadili.
Alivitaka vyombo vyote vinavyohusika kuhakikisha hoja za CAG zinafanyiwa kazi kwa wakati, ili halmashauri iendelee kutoa huduma bora kwa wananchi.
Hatua ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kuagiza Halmashauri ya Namtumbo kuongeza kasi ya kushughulikia hoja za CAG ni ishara ya uongozi makini unaojali uwazi, uadilifu na uwajibikaji.
Ni wito kwa watumishi wa umma, madiwani na wadau wote kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika vizuri, hoja zinafungwa, na hatimaye huduma bora zinamfikia mwananchi wa kawaida.