Klabu ya Yanga SC imeendelea kupata pigo katika harakati zake za kupinga maamuzi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), ikiwemo uamuzi wa kuahirishwa kwa mchezo namba 184 dhidi ya Simba SC. Licha ya juhudi zake za kushinikiza kuvunjwa kwa Bodi hiyo, kutaka Katibu Mkuu wa TFF kujiuzulu, na kutotambua rasmi mchezo huo, Bodi ya Ligi imesimama kidete na kupangia tarehe mpya ya mchezo huo kuwa Juni 25, 2025.
Yanga SC, kupitia taarifa zake kutoka kwa Afisa habari wake Ali Kamwe amenukuliwa mara kadhaa akikataa katakata kutambua mchezo namba 184 na kudai kuwa hawatacheza na hata michezo mingine iliyobaki ya Ligi Kuu hawatacheza
Ali Kamwe alifika mbali wakati alipotoa taarifa kuwa hata mchezo wa Fainali wa Kombe la CRDB unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni Zanzibar hawatacheza kwa sababu wanalidai shirikisho la. mpira wa migu fedha za zawadi ya ushindi wa Kombe hilo.
Jambo lililopelekea Benki ya CRDB na TFF kutolea ufafanuzi jambo hilo, Afisa habari huyo pia alieleza kuwa hawaridhishwi na namna TPLB na TFF walivyoshughulikia suala hilo, akidai kuwa haki haikutendeka. Klabu hiyo imeweka bayana kuwa haitambui uhalali wa mchezo namba 184, ikihusisha maamuzi hayo na kile wanachodai kuwa ni “upendeleo” wa wazi kwa timu pinzani.
Taarifa rasmi kutoka TPLB imethibitisha kuwa mchezo kati ya Simba SC na Yanga SC sasa utafanyika tarehe 25 Juni 2025, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam. Bodi hiyo imesisitiza kuwa imefanya maamuzi hayo kwa mujibu wa kanuni za ligi na ratiba ya mashindano, huku ikitoa wito kwa pande zote kuheshimu taratibu za mchezo wa soka.
Awali kabla ya kusogezwa mbele kwa mchezo huo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan alikutana na viongozi wa klabu ya Simba na Yanga ikulu Chamwino leo Juni 13, 2025 na kuzungumza nao na baada ya mazungumzo hayo Bodi ya Ligi ikatoa taarifa ya kusogeza mbele kwa mchezo huo namba 184.
Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Yanga SC kushindwa katika jitihada zake za kupinga maamuzi ya vyombo vya uongozi wa soka nchini baada ya kuangukia pua pia katika Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo CAS huko Zurich Uswiss, jambo linaloibua mjadala mpana miongoni mwa wadau wa michezo kuhusu sakata hilo la Yanga bodi ya Ligi na TFF