Na Farida Mangube Morogoro
Jamii imetakiwa kuwajali na kuwathamini wazee, hasa wale wasiojiweza, kama ishara ya kutambua mchango wao katika ujenzi wa taifa.
Wito huo umetolewa na baadhi ya wasanii wa muziki na filamu nchini waliotembelea na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali katika kituo cha kulelea wazee cha Funga Funga kilichopo mkoani Morogoro.
Wasanii hao wakiongozwa na Taasisi ya MMASUTA chini ya uongozi wa Cleopas Msuya, walipeleka msaada kwa wazee hao ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao kwa taifa.
“Wazee hawa walifanya mambo makubwa wakiwa na nguvu, leo hii wanahitaji kutunzwa. Tumeona ni vyema kuwapa moyo na kuwasaidia kwa kile kidogo tulichonacho,” alisema Msuya.
Miongoni mwa wasanii walioshiriki ni Ahmed Olotu maarufu kama Mzee Chilo pamoja na Rasia Makuka, waliotoa wito kwa wasanii wenzao na watu binafsi wenye uwezo kuiga mfano huo kwa kuwasaidia wazee wanaoishi katika mazingira magumu.
“Wazee ni hazina ya taifa. Tukiwasahau tunapoteza misingi yetu. Tunawaomba Watanzania wengine waone umuhimu wa kutoa msaada kwa wazee wetu,” alisema Mzee Chilo.
Kwa upande wake, mmoja wa wazee wanaoishi kituoni hapo, Osea Daniel, alishukuru kwa msaada huo na kueleza kuwa umetia moyo kwa wazee wanaohisi wamesahaulika.
“Tunawashukuru sana kwa kutukumbuka. Tumefarijika kuona bado tunathaminiwa,” alisema kwa hisia.
Kituo hicho, ambacho kilianzishwa mwaka 1945 kwa lengo la kuwahudumia wazee wasio na uwezo wa kujikimu, kwa sasa kinalea wazee 19 wanaohitaji huduma za msingi za kila siku.