Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imeandaa Sheria, Sera na Mipango ya kitaifa ili kuwajengea uwezo Vijana Nchini.
Mkurugenzi Idara ya maendeleo ya Vijana Zanzibar Shaib Ibrahim Mohammed ameyasema hayo wakati akifunguwa mafunzo ya Stadi za maisha kwa Vijana kutoka Taasisi mbalimbali huko Bweleo Wilaya ya Magharibi B.
Amesema, Idara hiyo, ina jukumu la kuratibu na kusimamaia maendeleo ya Vijana ili kuyatekeleza mambo yaliomo katika Sera na mipango ya kitaifa kwa maslahi ya Vijana na Taifa kwa Ujumla.
Aidha amesema mafunzo ya Stadi za maisha, yatasaidia kupunguza au kutondosha vitendo vya Udhalilishaji, Utumiaji wa Dawa za kulevya na Mmongonyoko wa maadili nchini.
Hata hivyo amesema mafunzo hayo, yatawawezesha Vijana kuwa na Mawasiliano mazuri na kujenga mtandao wa pamoja hasa katika kipindi hiki cha sayansi na teknolojia.
Mratibu Idara ya maendeleo ya vijana Zanzibar Salma Kombo Mohammed amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo Vijana ili waweze kujitegemea.
Ambapo mratibu wa kituo cha mafunzo ya vijana Bweleo Massoud Juma Haji amesema Mafunzo hayo, yatasaidia kuwajenga vijana kuwa na mtazamo mwema na kupata mawazo mazuri, yatakayopelekea mustakbali mwema wa maisha yao ya sasa na baadae.
Nao Vijana waliopatiwa mafunzo hayo, wameishukuru Idara ya maendeleo ya vijana Zanzibar kwa kuwapatia elimu hiyo na kuahidi kuyafikisha kwa wenzao ili kuleta mwamko kwa jamii.
Mafunzo hayo ya siku 5 ya Stadi za maisha, yameandaliwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kupitia Idara ya Maendeleo ya Vijana chini ya ufadhili wa Shirika la Idadi ya Watu Ulimwenguni (UNFPA) na kushirikisha Taasisi mbalimbali zinazohusiana na masuala ya Vijana Nchini.