Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, mkoani Mara, imefanikiwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha, kutoka lengo la awali la Shilingi bilioni 4.7 na kufikia Shilingi bilioni 5.8.
Mafanikio hayo yamepongezwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee Mtambi, alipokuwa akihutubia Baraza la Madiwani wakati wa majadiliano ya hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
RC Mtambi ameitaka Halmashauri hiyo kuhakikisha kuwa fedha zote zinazokusanywa kutoka kwenye mapato ya ndani zinawekwa benki kwa mujibu wa sheria na taratibu za kifedha za serikali.
Aidha, ameiagiza Halmashauri kuimarisha usimamizi wa vyanzo vya mapato vilivyopo, hususan vile ambavyo havijalindwa ipasavyo, ili kuongeza mapato ya ndani kwa ajili ya shughuli za maendeleo na uendeshaji wa Halmashauri.
Kwa upande wao, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayubu Makuruma, pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, wameahidi kuendelea kuboresha na kuimarisha usimamizi wa mapato, hususan katika maeneo yanayozunguka Hifadhi, ili kuhakikisha makusanyo yanaongezeka na kuwanufaisha wananchi.