Dar es Salaam, Juni 10, 2025.
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeweka alama mpya ya uongozi bora na uwajibikaji katika taasisi za umma baada ya kuchangia Shilingi bilioni 300 kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, hatua iliyotambuliwa kwa tuzo maalum kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan.
Tuzo hiyo ya heshima ilikabidhiwa kwa Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, katika hafla rasmi ya utoaji wa gawio na michango ya mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa, iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
BoT imekuwa mfano wa taasisi yenye uwajibikaji wa hali ya juu na usimamizi thabiti wa rasilimali za taifa, hali iliyoifanya kuibuka kama miongoni mwa wachangiaji wakubwa wa mapato yasiyo ya kikodi kwa Serikali katika mwaka wa fedha 2024/2025.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia alieleza kuwa mchango wa BoT ni wa kipekee na unaonyesha namna taasisi za umma zinavyoweza kuleta matokeo chanya pale zinapotekeleza majukumu yao kwa uadilifu, weledi na ubunifu.
“Benki Kuu imethibitisha kuwa taasisi za umma zina uwezo mkubwa wa kuongoza mageuzi ya kiuchumi endapo kutakuwa na usimamizi thabiti na dhamira ya kweli ya kulitumikia taifa,” alisema Rais Samia.
Kwa upande wake, Gavana Tutuba alisema mafanikio hayo yametokana na mageuzi ya kiutendaji ndani ya BoT pamoja na ushirikiano mzuri na taasisi nyingine za Serikali, akisisitiza kuwa benki hiyo itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuchangia maendeleo ya Taifa.
Mchango wa BoT unaifanya kuwa taasisi ya kipekee kati ya taasisi zote zilizotoa gawio na michango mwaka huu, jambo lililowapa heshima ya kutunukiwa tuzo maalum, tofauti na tuzo za makundi yaliyotolewa kwa mashirika mengine.