Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Juni 8,2025
Viongozi 20 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini, mkoani Pwani—wakiwemo Wenyeviti, Makatibu na Makatibu wa Jumuiya mbalimbali—wameachia nafasi zao wakitarajia kugombea Udiwani wa Kata pamoja na Viti Maalum katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo, Katibu wa CCM Wilaya ya Kibaha Mjini, Issack Kalleiya, alisema viongozi hao wamefuata taratibu stahiki za chama kabla ya kuachia nafasi zao.
“Mimi kama msimamizi wa kanuni katika wilaya, natambua kuwa viongozi hao wamefuata utaratibu wa chama, Chama kina taratibu, katiba, kanuni na miongozo ambayo wanapaswa kuiheshimu,” alisema Kalleiya.
Hata hivyo, alitoa angalizo kuwa pamoja na kujiuzulu, viongozi hao hawaruhusiwi kuanza kampeni kabla ya muda rasmi kuruhusu kufanya hivyo.
“Sasa wao wamepisha ,hatua inayofuata ni kwenda kupata wajumbe wengine watakaochukua nafasi zao ili baadae vikao viweze kujadili , maana unawezakuta watu wanne ama watano walikuwa wajumbe wa kamati ya siasa, hivyo kama wamepisha lazima wapatikane wengine watakaoziba mapengo “alieleza Kalleiya.
Aidha, Kalleiya aliwasihi wenye nia ya kugombea kushikamana na kufuata taratibu za chama, bila kuleta vurugu au kuanzisha makundi ya kisiasa yatakayohatarisha utulivu wa wilaya.
“Wasitengeneze makundi ya vurugu, wasubiri mchakato rasmi wa kuchukua na kurejesha fomu utakapofunguliwa, Wilaya yetu bado iko salama, changamoto zilizopo ni ndogo na za kawaida hasa kuelekea kipindi cha uchaguzi,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa ni jambo la kawaida kwa makundi kujitokeza katika hatua za mchakato wa uchaguzi, lakini alisisitiza kuwa hayapaswi kusababisha mgawanyiko au kuathiri mshikamano ndani ya chama.
“Nawasihi pia wasikubali kushawishiwa na zawadi au ahadi zisizo rasmi ambazo zinaweza kuchochea vurugu, Waendelee kuwa watulivu hadi pale utaratibu wa chama utakaporuhusu hatua zinazofuata,” alionya.
Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi ya CCM mwaka 2025, kuchukua na kurejesha fomu za kugombea Udiwani,Wadi, Ubunge, Uwakilishi na Viti Maalum kutafanyika kuanzia Juni 28 hadi Julai 2 mwaka huu.
Vikao vya uchujaji wa wagombea vitaanza Julai 4,2025 kabla ya kufanyika kwa kura za maoni.