Na Sophia Kingimali,Dar es salaam.
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, amewataka vijana waliomaliza vyuo nchini na ambao bado wapo vyuoni kuwahasisha vijana waliotimiza umri wa kupiga kura kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kumchagua Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ili aweze kuendelea kuwatumikia wananchi.
Pia,amesema Bunge litaendelea kuishauri na kuisimamia Serikali kushughulikia kwa haraka changamoto ya ucheleweshaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, huku akisisitiza kuwa elimu ni kipaumbele katika ajenda ya maendeleo ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Akizungumza leo June 6,2025 kwenye Mahafali ya nane ya Seneti ya Vyuo na Vyuo Vikuu Mkoa wa Dar es Salaam, Dkt. Tulia amesema kuwa Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu, na kwamba Bunge litaendelea kulifuatilia suala la utoshelevu wa mikopo ili kuhakikisha wanafunzi wote wenye uhitaji wanapata huduma hiyo kwa wakati.
“Tutaendelea kuishauri Serikali pamoja na Waziri wa Elimu ili kuhakikisha changamoto ya ucheleweshwaji wa mikopo inapatiwa ufumbuzi wa kudumu,” amesema Dkt. Tulia.
Aidha, amesisitiza kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinawathamini wasomi na kila mmoja ndani ya jamii, na kwamba maoni ya wananchi, hasa vijana, yamekuwa yakizingatiwa na kufanyiwa kazi na chama hicho tawala.
“Tunaenda na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sababu maeneo mengi ameyawezesha, hususan katika elimu. Ni CCM pekee yenye uwezo wa kusogeza maendeleo haya mbele zaidi. Oktoba nenda ukapige kura, mchague Samia na viongozi wengine wa CCM,” ameongeza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Nasra Ramadhani, amesema Mkoa uko salama kisiasa na vijana wameshiriki kikamilifu katika michakato yote ya uchaguzi ikiwemo uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
“Tunayo mahusiano mazuri kati ya chama, taasisi za elimu ya juu na halmashauri zetu. Kupitia asilimia 10 za mapato ya ndani, vijana wamewezeshwa kiuchumi,” amesema.
Akichangia kwenye hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema mfumo wa “KKK – Kula, Kulala, Kusoma” umeongezewa maana kwa kuongeza “Kusoma kwa bidii huku ukifanya kazi”, akibainisha kuwa viwanda vitaanza kuchukua wanafunzi kama hitaji la kisheria.
“CCM imetambua kuwa ajira bado ni changamoto, ndiyo maana kwenye ilani ya chama ya 2025/30 tumepanga kila mtaa uwe na viwanda,” amesema Profesa Mkumbo.