Na Meleka Kulwa, Dodoma
Wakati Serikali ikiendelea na juhudi za kuboresha elimu nchini, imetangazwa rasmi kuwa jumla ya wanafunzi 214,141 wakiwemo wasichana 97,517 na wavulana 116,624 wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo vya Elimu ya Ufundi kwa mwaka wa masomo 2025, baada ya kukamilika kwa mchakato wa uchaguzi wa wanafunzi uliozingatia Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (toleo la 2023) pamoja na mtaala ulioboreshwa.
Taarifa hiyo imetolewa kwa waandishi wa habari na Waziri wa Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati wa mkutano uliofanyika jijini Dodoma, ambako viongozi kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI na wadau wa elimu walikutana kutangaza rasmi matokeo ya uchaguzi huo muhimu kwa mustakabali wa elimu nchini.
Waziri Mchengerwa ameleza kuwa kati ya wanafunzi waliochaguliwa, 149,818 wamepangwa katika shule za sekondari za Serikali zipatazo 694, ambapo wanafunzi 1,728 walipangwa katika shule nane (8) zenye ufaulu wa juu zaidi, 141,146 katika shule za bweni, na 6,944 katika shule za kutwa.
Aidha, ameeleza kuwa wanafunzi 2,875 wamechaguliwa kujiunga na fani mbalimbali katika vyuo vinne vya elimu ya ufundi ambavyo ni:
Chuo cha Ufundi Arusha (ATC)
Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT)
Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST)
Chuo cha Maendeleo ya Maji (WMDI)
Vilevile, 2,214 watajiunga na vyuo vya afya (ngazi ya stashahada), 1,609 vyuo vya ualimu, na 57,625 katika vyuo vya kada mbalimbali.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotangazwa, muhula wa kwanza kwa wanafunzi wa Kidato cha Tano utaanza tarehe 08 Julai, 2025, huku siku ya mwisho ya kuripoti shuleni ikiwa ni tarehe 21 Julai, 2025.
Waziri Mchengerwa alisisitiza kuwa uchaguzi umezingatia ufaulu wa wanafunzi na nafasi zilizopo, na kwamba hakutakuwa na nafasi ya mabadiliko ya shule kwa wanafunzi waliopangiwa tayari. Pia, Serikali imesisitiza kuwa maelekezo ya kujiunga kwa waliochaguliwa kujiunga na vyuo vya elimu ya ufundi yatatolewa moja kwa moja na vyuo husika.
Aidha, pongezi zimetolewa kwa walimu, wazazi na walezi kwa jitihada zao zilizowezesha ongezeko la ufaulu kwa wanafunzi, ambapo takwimu zinaonesha kuwa ufaulu wa daraja la I–III umeongezeka kwa 5.36% kutoka asilimia 35.87 mwaka 2023 hadi asilimia 41.23 mwaka 2024.
Katika kuendeleza juhudi za Serikali za kuhakikisha fursa za elimu zinapatikana kwa wote, viongozi wa Serikali wamehimiza ujenzi na upanuzi wa shule za Kidato cha Tano katika kila Tarafa nchini pamoja na kuongeza tahasusi za Sayansi, ili kupunguza gharama za usafiri na kuongeza uwiano wa elimu kwa mikoa yote.
Kwa taarifa zaidi, orodha kamili ya wanafunzi waliochaguliwa na fomu za kujiunga zinapatikana katika tovuti rasmi za: www.tamisemi.go.tz www.nactvet.go.tz