Mwanga, Kilimanjaro – Juni 5, 2025
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ameidhinisha rasmi uanzishwaji wa Shule ya Sekondari ya Amali katika eneo la Kilaweni, Usangi – wilayani Mwanga, mkoa wa Kilimanjaro. Hatua hiyo imekuja baada ya kufanya ziara ya kikazi kukagua maendeleo ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari inayojengwa katika eneo hilo.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkenda aliambatana na viongozi wa wilaya pamoja na Mbunge wa Mwanga, Mhe. Joseph Tadayo, ambaye aliwasilisha ombi la wananchi wa Mwanga kutaka shule hiyo ibadilishwe na kuwa shule ya amali ili kuwapa vijana ujuzi wa vitendo utakao wawezesha kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.
Baada ya kuridhishwa na kasi na ubora wa utekelezaji wa mradi huo, Prof. Mkenda alikubaliana na ombi hilo na kutoa maelekezo kwa wataalamu kutoka Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kuanza mara moja mchakato wa mapitio ya mradi ili kuingiza mtaala wa elimu ya amali.
> “Tumepokea ombi lenu. Serikali inatambua umuhimu wa elimu ya amali, na shule hii itakuwa sehemu ya mpango wa kitaifa wa kuimarisha ujuzi wa vijana wetu. Nimeagiza VETA waanze kazi mara moja ili shule hii iwe mfano wa mafanikio ya elimu ya amali nchini,” alisema Prof. Mkenda.
Wananchi waliokusanyika kushuhudia ziara hiyo walilipuka kwa shangwe na vifijo kufuatia uamuzi huo, wakieleza kuwa shule hiyo itakuwa mkombozi mkubwa kwa vijana wa Mwanga na maeneo jirani.
Uamuzi huu unaendana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwekeza katika elimu yenye tija kwa kizazi cha sasa na kijacho.