Na Sophia Kingimali.
Chama cha ACT Wazalendo kimempokea mwanachama mpya wa chama hiko Shekh Ponda Issa Ponda huku wakiwa na matumaini makubwa nae katika kukijenga chama lakini pia katika harakati zake za kutetea na kuwaletea maendeleo wananchi.
Akizungumza mara baada ya kumpa kadi ya chama leo june 5,2025 jijini Dar es salaam Kiongozi wa ACT Dorothy Semu amesema wanaimani kubwa na Shekh ponda katika kukiimarisha chama kwani ujio wake utaongeza nguvu ya mabadiliko.
“Shekh Ponda ni mwamba wa harakati nchini tumempokea kwa furaha lakini pia tunamshukuru kwa kukipa chama chetu heshima na niimani yangu kuwa kuingia kwake katika chama kutaongeza katika mapambano yetu ya kutetea demokrasia ya nchi yetu”,Amesema.
Akizungumza mara baada ya kupokea kadi ya chama Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania ,Sheikh Ponda Issa Ponda amesema amechukua kadi akiwa na lengo kuu la kujiimarisha kisheria ili kupata jukwaa la kuwaelimisha wananchi wajue ajenda kuu ya Taifa lao lakini pia kuwahamasisha wananchi kupigania mambo ya msingi.
“Ndugu zangu mapambano ya kudai haki si ta mtu mmoja wala chama kimoja cha siasa,viongozi wa dini bali kila mtanzania anaejali mustakabali wa Taifa lake”,amesema.
Sambamba na hayo ametoa wito kwa viongozi wa dini kushiriki katika siasa kwani uwepo wao katika vyombo vya maamuzi ni muhimu na utalinda maadili ya utu na Taifa.
upande wake Katibu Mkuu wa Chama hicho Ado Shaibu amesema wamefurahia sana na ujio wa Sheikh Ponda katika chama chao kwani kila jambo linawakati wake.
Amesema Sheikh Ponda anafahamika kwa mengi katika uwanja wa siasa na jina lake sio ngeni kwani kuna nyakati alipanda katika majukuwaa mbalimbali ya kisiasa ikiwemo Chama cha Wamanchi CUF pamoja na Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA.
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania ,Sheikh Ponda Issa Ponda akabidhiwa rasmi kadi ya heshima ya Maalim Seif ya Chama cha Act Wazalendo huku akisisitiza kuchangia nguvu katika Operesheni ya ACT Wazalendo ya Linda Demokrasia, inayolenga kurejesha haki, uwazi, na usawa katika michakato ya uchaguzi nchini Tanzania.
Mapokezi hayo ya Sheikh Ponda yameongozwa na Kiongozi wa Chama hicho Dorothy Semu pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Chama hicho pamoja na Ngome zake .