NIRC:Igunga
Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), imeingia mkataba na mkandarasi mzawa kampuni ya Samota limited kujenga mradi wa skimu ya umwagiliaji Mwamapuli, katika kijiji cha Mwanzugi wilayani Igunga mkoani Tabora, mradi ambao utagharimu zaidi ya shilingi bilioni 26.9.
Aidha mradi huo utajengwa kwa zaidi ya siku 720, ukiwa unalenga kuongeza eneo la umwaagiliaji kutoka hekta 630 , hadi kufikia hekta 2397, huku zaidi ya wakulima 2470 wakitarajiwa kunufaika kutokana na mradi huo
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Paul chacha, amemtaka mkandarasi mzawa kampuni ya Samota LTD, anayetekeleza mradi huo kufanya kazi kwa ufanisi na kwa muda wa makubaliano.
Alisema ni muhimu mkandarasi huyo kuheshimu makubaliano na kuzingatia uhitaji wa wananchi
“Serikali ina nia njema lengo ni mradi umalizike kwa wakati ili uweze kuanza kuwanufaisha wananchi,”alisema.
Akisoma taarifa ya ujenzi wa mradi huo Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Tabora Francis Mgangalula alisema utakelezaji wa mradi huo utahusisha shughuli mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara za mashambani,ujenzi wa ofisi ya Tume, nyumba ya meneja wa skimu pamoja na ununuzi wa gari moja kwa ajili ya usimamizi wa mradi.
“Mradi huu ni mkubwa ambao serikali imewekeza fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wake, niwasihi wananchi mara baada ya kukamilika, tuutunze kwa ajili ya kilimo endelevu,”alisema.
Naye mwakilishi kutoka kampuni ya Samota Ltd Ahmed Salumu, ameahidi kutekeleza mradi huo kwa wakati na ubora unaotakiwa, kama ilivyokusudiwa na Serikali.