Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akishiriki Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika kuhusu hali ya Kipindupindu Barani Afrika uliyofanyika kwa njia ya mtandao. Tarehe 04 Juni 2025 Dodoma.
……..
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika kuhusu hali ya Kipindupindu Barani Afrika uliyofanyika kwa njia ya mtandao.
Mkutano huo ulioandaliwa na Kituo cha Afrika cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa umeshirikisha Wakuu wa Nchi na Serikali, Viongozi mbambali katika sekta ya afya, maji na fedha pamoja na mashirika ya Kimataifa ikiwemo Shirika la Afya Duniani na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF).
Akizungumza katika Mkutano huo, Makamu wa Rais amesema katika kukabiliana na ugonjwa wa Kipindupindu, Bara la Afrika linahitaji kuzalisha chanjo, bidhaa za afya pamoja na kuwa na mifumo ya uangalizi itakayoweza kutambua mapema viashiria vya ugonjwa huo.
Pia ametoa wito wa kuimarishwa kwa mifumo ya Afya pamoja na kuhakikisha amani inapatikana katika maeneo yenye migogoro barani Afrika ili kuweza kupambana na ugonjwa huo pamja na kuifikia jamii inayoathirika na ugonjwa huo kirahisi.
Amesisitiza kutumia mbinu za kushirikisha sekta mbalimbali ili kupata suluhu endelevu ya kupambana na ugonjwa huo pamoja na kuzuia mlipuko wa magonjwa mengine.
Amesema mpango wa ushirikishaji wa sekta uhakikishe uhakika wa maji safi na salama, vyoo bora, usimamizi bora wa taka, elimu jumuishi ya jamii kuhusu usafi kama vile uchemshaji maji na unawaji mikono mara kwa mara.
Makamu wa Rais ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa na Umoja wa Mataifa kufanya kazi kwa karibu na Umoja wa Afrika kuhakikisha inatoa kipaumbele katika kutokomeza ugonjwa wa kipindupindu kulingana na malengo ya Shirika la Afya Duniani ya kupunguza ugonjwa huo kwa asilimia 90 ifikapo mwaka 2030.
Makamu wa Rais amesema pamoja na kwamba ugonjwa wa kipindupindu unazuilika na kutibika lakini bado umeendelea kuathiri watu wengi barani Afrika ambapo kufikia mwezi Mei mwaka 2025 inakadiriwa jumla ya watu 2600 wamepoteza Maisha kutokana na ugonjwa huo.
Aidha amesema katika kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu, Tanzania imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuunganisha nguvu ya pamoja kwa kushirikisha sekta zote muhimu katika kukabliana na hali hiyo pamoja na kutumia rasilimali za ndani katika kupambana na ugonjwa huo.
Pia ametaja hatua zingine ni pamoja na kuhamasisha ushiriki wa jamii katika kukabiliana na janga hilo kupitia kampeni mbalimbali za afya ya jamii kwa kutumia vyombo vya habari, viongozi wa kijamii, dini na mila pamoja na kuanzisha elimu na mafunzo ya usafi kupitia programu mbalimbali mashuleni.
Wakuu wa Nchi na Serikali walioshiriki Mkutano huo, wamesisitiza kuwepo kwa juhudi za pamoja katika kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu ikiwemo kubadilishana maarifa na taarifa muhimu pamoja na mbinu mbalimbali za kujikinga na kutokomeza ugonjwa huo.