NIRC Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Ushirika na Umwagiliaji, Dkt. Stephen Nindi, ameitaka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kutanua wigo wa kazi zake kwa kuwafikia wadau jumuishi wa sekta nyingine lengo likiwa ni kuhakikisha kilimo cha umwagiliaji kinakuwa na tija katika maendeleo ya jamii.
Nindi amesema hayo alipotembelea banda la Tume ya Taifa ya Umwagiliaji viwanja vya Jakaya Kikwete jijini Dodoma katika maadhimisho ya wiki ya Mazingira Duniani.
Dkt. Nindi amesema kuwa pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Tume, ni vyema taasisi hiyo muhimu katika sekta ya kilimo ikaendelea kutanua wigo ili kuwafikia wadau wengine, mbali na wakulima wa mazao pekee.
“Wakulima wa umwagiliaji si tu wanajikita kwenye kilimo, bali pia wanajihusisha na uvuvi, ufugaji na matumizi ya maji ya nyumbani. Ni muhimu kuweka mikakati inayozingatia uhitaji huu mtambuka ili kuongeza tija na matumizi endelevu ya rasilimali,” amesema Dkt. Nindi.
Katika kuendeleza juhudi za utunzaji wa mazingira, Mkuu wa Kitengo cha Mazingira wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Fumba Malima, ameeleza kuwa Tume inaendelea na mipango mikakati endelevu ya kulinda mazingira katika skimu za umwagiliaji nchini.
Amesema, Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kusisitiza umuhimu wa utunzaji wa mazingira kama sehemu ya mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Wataalamu wetu wanatoa elimu kwa wakulima juu ya namna bora ya kutunza mazingira na kuteketeza taka za plastiki zinazotokana na matumizi ya viuatilifu na mbolea. Lengo ni kuhakikisha miradi ya umwagiliaji inazingatia usalama wa afya za watu na mazingira,” amesema Malima.
Malima, amesisitiza kuwa NIRC ikiwa mdau wa mazingira nchini itaendelea kuhakikisha miradi yake na utendaji unazingatia kanuni, sheria na matakwa ya kidunia katika utunzaji wa mazingira, hivyo ametoa wito kwa wadau wa maonyesho hayo kufika katika banda la Tume ili kupata elimu.
“Maonyesho haya ni muhimu kwa kuwa yanandelea kuhamasisha wadau mbalimbali kushiriki katika utunzaji wa mazingira. Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetumia fursa hii kuhamasisha umuhimu wa kilimo cha umwagiliaji kinachozingatia utunzaji mazingira kwa maendeleo endelevu,”amesema,
Maadhimisho ya Wiki ya Mazingira Duniani yanaendelea katika Viwanja vya Jakaya Kikwete, Dodoma na kilele kinatarajiwa kuwa kesho Juni 5 2025, ambapo viongozi na wadau mbalimbali wanatarajiwa kushiriki huku Kaulimbiu ya Wiki ya Mazingira Duniani mwaka huu ikiwa “Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo, Tuwajibike Sasa; Dhibiti Matumizi ya Plastiki;