Na WMJJWM-Dar Es Salaam
Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini wameaswa kupaza sauti katika kuelimisha jamii juu ya utekelezaji wa Programu ya Kizazi chenye Usawa yenye lengo la kuleta Usawa wa Kijinsia katika nyanja mbalimbali.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum anayeshugulikia Maendeleo ya Jinsia na Wanawake Felister Mdemu wakati akifungua kikao kati ya Wizara na Wahariri wa Vyombo mbalimbali vya habari Juni 03, 2025 jijini Dar Es Salaam.
Felister amesema kuwa Vyombo vya Habari ni mojawapo ya wadau wakubwa katika kuhakikisha kuwa taarifa za utekelezaji wa Programu hii zinawafikia walengwa. Hivyo suala hilo likibebwa kwa pamoja na dhamira ya dhati katika kusambaza taarifa sahihi za utekelezaji wa Programu kwa kuweka ahadi mahsusi kwenye maeneo ya utekelezaji.
Felister amesema Wahariri ni kundi ambalo linafikia jamii kwa haraka na kubadilisha fikra na mitazamo hivyo amewaasa kutumia vyombo vyao vya habari ili kupaza sauti juu ya utekelezaji wa Programu ya Kizazi chenye Usawa katika jamii.
“Niseme tu ninyi ni muhimu katika kufikisha masuala mbalimbali katika jamii tulibebe na hili la Usawa wa Kijinsia tukaielimishe jamii ila tuweze kufikia malengo ya kuwa na Kizazi chenye Usawa nchini” amesema Felister
Aidha amesema lengo la kikao hicho ni kuwawezesha wahariri kuhariri na kusanifu taarifa zinazohusiana na Programu ya Kizazi Chenye Usawa kabla hazijarushwa na kutolewa katika vyombo vya habari ili jamii ipate kuelewa kwa kina masuala ya haki na usawa wa kiuchumi.
“Hivyo basi, nawasihi tushiriki kwa kujadili kikamilifu ili tufikie matokeo tarajiwa ya kuboresha zaidi Utekelezaji wa programu ikiwa ni pamoja na changamoto zinazotukabili na kupanga mipango endelevu katika kuleta usawa wa haki za kiuchumi katika jamii zetu.” amesema Felister
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Utekelezaji wa Programu ya Kizazi chenye Usawa Mhe. Angelah Kairuki amewaomba Wahariri wa Vyombo mbalimbali vya habari kuweka mkazo wa habari zinazohusu Kizazi chenye Usawa ili ziwafikie wananchi.
Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Deodatus Balile amesema Jukwaa litahakikisha kuwa utekelezaji wa Programu ya Kizazi chenye Usawa onazungumzwa kupitia vyombo vya habari ili kuonesha uzuri wa uwepo wa Usawa wa Kijinsia katika jamii katika nyanja mbalimbali za Maendeleo.
Naye Naibu Mwakilishi Mkazi UN Women Katherine Gifford amesema wataendelea kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali kuhakikisha agenda ya Kizazi chenye Usawa inaeleweka na kuwafikia wananchi, ili kufikia Azma ya kuwa na Kizazi chenye Usawa Tanzania.