Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Katika siku ya pili ya Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wajumbe wa mkutano huo walipokea salamu za mshikamano na pongezi kutoka kwa wawakilishi wa vyama rafiki na mataifa mbalimbali duniani. Salamu hizo zilieleza uhusiano wa kihistoria, ushirikiano wa kimkakati na mshikamano wa kindugu uliopo kati ya CCM na vyama hivyo.
Vyama rafiki vilivyoshiriki kuwasilisha salamu zao vinatoka katika nchi za Uganda, Urusi, China, Zimbabwe, Malawi, Angola, Rwanda, Zambia, Burundi, Cuba na Namibia. Uwakilishi huu wa kimataifa unaakisi nafasi ya CCM katika majukwaa ya kisiasa ya kimataifa na jinsi ambavyo chama hicho kinathaminiwa na kushirikiana kwa karibu na vyama vya ukombozi na maendeleo duniani.
Wawakilishi wa vyama hivyo walitumia fursa hiyo kuipongeza CCM kwa mafanikio yake katika kuendeleza amani, utulivu na maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania. Aidha, walisisitiza umuhimu wa kuendeleza mshikamano baina ya vyama vyao kwa lengo la kuimarisha misingi ya haki, uhuru, na maendeleo endelevu.
Salamu hizo zilipokelewa kwa shangwe na wajumbe wa mkutano, wakionyesha furaha na shukrani kwa uhusiano huo wa muda mrefu.