Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Mei 30, 2025, ametoa maagizo mahsusi kwa Katibu Mkuu wa CCM kuhusu mchakato wa uteuzi wa wagombea kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Agizo hilo limetolewa wakati wa hotuba yake kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM uliofanyika jijini Dodoma, ambapo pia alizindua Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kipindi cha 2025–2030.
Katika hotuba yake, Rais Samia alielekeza wazi kuwa majina ya wanachama wanaotaka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya CCM yawasilishwe kwake ifikapo tarehe 1 Juni 2025. Alisisitiza kuwa hakuna mwanachama anayepaswa kuwasilisha jina lake kwa madai ya kuungwa mkono na yeye binafsi au Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi. Alibainisha kuwa nafasi maalum kumi za uteuzi zitashughulikiwa na viongozi hao baada ya uchaguzi mkuu.
“Ninamuagiza Katibu Mkuu kuhakikisha kuwa majina ya wanaotaka kugombea yamefika mezani kwangu kabla ya tarehe 1 Juni. Hakuna mgombea anayekuja kwa baraka zangu wala za Rais wa Zanzibar. Tutasimamia uteuzi baada ya uchaguzi kwa nafasi zinazotuhusu,” alieleza Rais Samia kwa msisitizo.
Aidha, Rais Samia alisisitiza umuhimu wa Katibu Mkuu kusimamia mchakato wa uteuzi kwa uwazi, haki, na uadilifu ili kuhakikisha kuwa wanapitishwa wagombea wenye uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Alionya dhidi ya kuteua wagombea kwa misingi ya uswahiba au mihemko ya kisiasa.
“Msilete mgombea kwa sababu ni mtu wa fulani. Tuleteeni wagombea wanaoweza kubeba majukumu na kuimarisha maisha ya Watanzania. Asiyefaa asipitishwe, anayefaa apewe nafasi yake. ‘Mcheza ngoma si yake, lazima ataharibu,’” alionya.
Maagizo hayo yametolewa sambamba na wito wa Rais kwa wanachama wa CCM kuhakikisha wanapeleka Ilani mpya kwa wananchi ili kuelewa yaliyomo na kuwashirikisha kikamilifu katika safari ya uchaguzi. Pia alihimiza mshikamano, umoja na maadili miongoni mwa wanachama hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Hotuba hiyo imeweka msingi wa uwajibikaji na uongozi bora ndani ya CCM huku ikisisitiza dhamira ya chama hicho kusimamia mchakato wa uteuzi kwa maslahi ya taifa.