Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Dodoma – Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo ameongoza Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika jijini Dodoma, huku chama hicho kikitangaza kuwapokea wanachama wapya Milioni 13.67 waliojiunga na chama hicho katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni.
Katika hotuba yake ya kufungua mkutano huo, Dkt. Samia aliwataka wanachama wapya na wa zamani kuendeleza mshikamano na maadili ya chama, akisisitiza umuhimu wa kuwa na chama imara chenye kuzingatia misingi ya haki, usawa na maendeleo kwa wote.
“Leo tunajivunia kuwa chama kikubwa si kwa idadi tu, bali kwa uimara wa misingi yetu. Kupokea wanachama wapya zaidi ya Milioni kumi na tatu ni ishara ya imani ya wananchi kwetu,” alisema Dkt. Samia mbele ya maelfu ya wajumbe waliohudhuria mkutano huo mkubwa.
Katibu Mkuu wa CCM, Emanuel Nchimbi alieleza kuwa zoezi la usajili wa wanachama wapya limefanyika kwa uwazi na kutumia mifumo ya kidijitali ili kuhakikisha uhalali na uwazi wa taarifa za wanachama hao wapya.
Mkutano huo pia umejadili ajenda mbalimbali zikiwemo tathmini ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, ambapo viongozi walihimizwa kuendelea kuwa karibu na wananchi.
Mkutano Mkuu huo umeendelea kuonesha uimara wa CCM katika ulingo wa siasa za Tanzania, huku viongozi wakiahidi kuimarisha zaidi uongozi, uwajibikaji na huduma kwa jamii, ili kuhakikisha chama kinaendelea kuwa na mvuto kwa kizazi cha sasa na kijacho.