Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia Miundombinu, Bw. Rogatus Mativila akiwa na wadua mbalimbali akikata utepe kama ishara ya uzinduzi wa mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya usalama barabarani iliyofanyika leo Mei 29, 2025, Dar es Salaam katika Shule ya Msingi Sinza Maalum, mradi huo unatekelezwa na Shirika la Amend Tanzania
………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imesema itaendelea kushirikiana na wadau kuhakikisha shule zote nchini zinakuwa maeneo salama kwa watoto, kwa kuhakikisha kunakuwa na uwepo wa vivuko vya watembea kwa miguu, matuta kwa ajili kupunguza mwendo pamoja na alama za barabarani.
Akizungumza leo Mei 29, 2025 Jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya usalama barabarani iliyofanyika Shule ya Msingi Sinza Maalum uliofanywa na Shirika la Amend Tanzania, Naibu Katibu Mkuu wa TAMISEMI anayeshughulikia Miundombinu, Bw. Rogatus Mativila, amesema kuwa watoto ni rasilimali muhimu ya Taifa, hivyo ni lazima jamii kujikite katika kuhakikisha wanatembea kwa usalama kwenda na kutoka shuleni kila siku.
Katika uzinduzi wa Shule hiyo miundombinu iliyowekwa ni pamoja na matuta ya kupunguza mwendo kasi, vivuko vya watembea kwa miguu, alama za barabarani pamoja na njia maalum za watembea kwa miguu katika eneo la Shule hiyo.
Bw. Mativila amesema kuwa ajali za barabarani zimeendelea kuleta huzuni kwa jamii, hasa watoto wanapopoteza maisha au kujeruhiwa katika mazingira ya shule.
“Si jambo la kawaida tena, ni wakati muafaka sasa kama Taifa kuanzisha mjadala wa kitaifa kuhusu namna ya kupambana na janga la ajali barabara kwa ajili ya kuwalinda watoto” amesema Bw. Mativila
Ametoa wito wa kuanzishwa kwa mjadala wa kitaifa kuhusu namna ya kudhibiti ajali za barabarani, huku akisisitiza kuwa vifo na majeruhi vinavyotokana haviwezi kuvumilika katika jamii ya Watanzania.
Mwakilishi wa Shirika la Amend Tanzania, Simon Kalolo, amesema kuwa
ajali za barabarani husababisha vifo vinavyokadiriwa kufikia milioni 1.3 duniani kila mwaka, huku wengine zaidi ya milioni 50 wakijeruhiwa, na kuwa chanzo kikuu cha vifo vya watoto na vijana wenye umri wa miaka mitano hadi 29.
Amesema kuwa kupitia mradi huo ambao ni mara ya kwanza kutekelezwa kwenye shule yenye wanafunzi wenye mahitaji maalum utawasaidia kwa asilimia kubwa.
“Tunafahamu changamoto wanazokutana nazo, na tunaamini maboresho haya si tu yatapunguza ajali, bali pia yatatia moyo kwa wazazi kupeleka watoto shuleni,” amesema Kalolo
Amesema kuwa Tanzania na Afrika kwa ujumla kuna takwimu za juu vya vifo barabarani licha ya kuwa na magari machache jambo ambalo linaonesha kwa kiasi gani tunapaswa kuchukua hatua za dharura.
Amefafanua mradi huo mpaka sasa umezifikia shule 59 nchini Tanzania, ikiwa ni sehemu ya shule 100 Afrika na kunufaisha wanafunzi zaidi ya 52,793 nchini na zaidi ya 102,000 Barani Afrika.
Ofisa Elimu wa Mkoa wa Dar es Salaam anayeshughulikia Elimu, Bw. Abedi Milanzi amesema kuwa mradi huo ni rafiki hivyo unakwenda kuwa msaada wa kupunguza changamoto za watoto wenye mahitaji maalum.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Jeshi la Polisi kutoka Kitengo cha Usalama Barabarani, SSP Mbunja Matibu, amesema kuwa jeshi hilo linaendelea kutoa elimu ya usalama kwa watoto na watu wazima.
Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Songoro Mnyonge , amesema kuwa tatizo la ajali limekuwa tatizo katika Manispaa ya Kinondoni, kwani hospital ya Rufaa ya Mwananyamala imekuwa ikipokea watu wanapoteza maisha kila siku kutokana na ajali barabarani.