NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Wekundu wa Msimbazi, Simba SC, wamefanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Singida Black Stars katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa leo Mei 28, 2025, kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Mchezo huo uliokuwa na ushindani mkali kutoka kwa pande zote, na ulimalizika kwa bao pekee lililofungwa na mshambuliaji Steven Mukwala dakika ya 42, akiunganisha pasi safi kutoka kwa kiungo mshambuliaji Jean Ahoua. Huku bao hilo lilidumu hadi filimbi ya mwisho.
Singida Black Stars walionyesha jitihada kupitia kwa mshambuliaji wao hatari, Jonathan Sowah, kinara wa mabao wa timu hiyo akiwa na mabao 11 hadi sasa.
Hata hivyo, juhudi zake mbili zilikwama mikononi mwa kipa wa Simba, Moussa Camara, ambaye aliokoa michomo hiyo kwa ustadi mkubwa.
Camara alionyeshwa kadi ya njano na mwamuzi Elly Sasii dakika ya 82 kwa kosa la kupoteza muda, huku Sowah naye akipewa kadi ya njano dakika ya 90 baada ya kumchezea faulo kipa huyo aliyekuwa akiokoa hatari langoni mwake.
Kwa ushindi huo, Simba SC wamefikisha pointi 72 na kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi, wakiwa nyuma ya vinara Yanga SC wenye pointi 73, huku timu zote zikicheza mechi 27.
Mabingwa hawa wa jadi wanatarajiwa kukutana uso kwa uso katika Kariakoo Dabi inayosubiriwa kwa hamu, itakayopigwa Juni 15, 2025, ikiwa ni mzunguko wa pili wa msimu wa 2024/25.