Mwanza, Tanzania
Benki ya NMB imethibitisha dhamira yake ya kuunga mkono maendeleo ya serikali za mitaa kwa kudhamini Mkutano Mkuu wa 25 wa Jumuiya ya Mamlaka za Serikali za Mitaa Ukanda wa Ziwa Viktoria (LVRLAC), uliofanyika jijini Mwanza.
Akitembelea banda la NMB katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange, alipata maelezo kutoka kwa Meneja Mwandamizi wa Huduma za Serikali wa NMB, Adelard Mang’ombo, kuhusu namna benki hiyo inavyoshirikiana na serikali za mitaa katika kuimarisha huduma za kifedha kwa jamii.
Katika kutambua mchango huo, Dkt. Dugange alimkabidhi cheti cha shukrani Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Faraja Ng’ingo, kwa niaba ya benki hiyo, kama ishara ya kuthamini udhamini wao katika mkutano huo muhimu. Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa LVRLAC, William Gumbo.
Akizungumza wakati wa mkutano huo, Dkt. Dugange aliipongeza NMB kwa kuwa mdau wa kweli wa maendeleo, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya sekta binafsi na serikali za mitaa katika kuinua maisha ya wananchi na kukuza uchumi wa maeneo ya pembezoni.
NMB imekuwa mstari wa mbele katika kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia huduma zake za kifedha, mikopo ya kimkakati, na elimu ya fedha kwa viongozi wa serikali za mitaa pamoja na wananchi.
Mkutano wa LVRLAC umeendelea kuwa jukwaa muhimu la kujadili changamoto na fursa za maendeleo katika ukanda wa Ziwa Viktoria, huku mwaka huu ukihusisha wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.