Nahodha wa timu wa Timu ya Mpira wa Miguu ya Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke Magesa J. Simirya (wa kwanza kushoto) akipokea zawadi mbalimbali kutoka kwa mgeni wa fainali ya mashindano hayo Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Comred Yese A. Wezza baada ya timu yake kuibua na ushindi wa bao 1–0 dhidi ya Boda Boda Buza FC katika mchezo wa fainali uliochezwa Mei 24, 2025 kwenye Uwanja wa TANESCO – Buza Sigara, Dar es Salaam. (PICHA NA NOEL RUKANUGA)
Afisa Usalama Mwandamizi wa TANESO Mkoa wa Temeke Bw. Steven Maganga akizungumza na wachezaji wa shirika hilo kabla ya kuanza kwa mchezo wa fainali ya Kombe la Boda Boda Super CUP 2025.
Benchi la Ufundi likiongozwa na Kocha wa TANESCO Temeke FC ambaye pia ni Kaimu Meneja wa TANESCO Wilaya ya Yombo, Bw. Stephen Kabuzole (wa kwanza kulia) wakijadili jambo wakati mchezo wa fainali ukiendelea.
Kikosi cha TANESCO Temeke Fc wakiwa katika picha ya pamoja.
Kikosi cha Boda Boda Buza FC wakiwa katika picha ya pamoja.
Picha za matukio mbalimbali.
………….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Timu ya Mpira wa Miguu ya Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Mashindano ya Kombe la UVCCM Boda Boda CUP 2025 baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1–0 dhidi ya Boda Boda Buza FC katika mchezo wa fainali uliochezwa Mei 24, 2025 kwenye Uwanja wa TANESCO – Buza Sigara, Dar es Salaam.
Goli hilo pekee limefungwa katika kipindi cha kwanza liliiwezesha TANESCO Temeke FC kutawala mchezo huo wa fainali kwa dakika zote 90, licha ya mashambulizi ya mara kwa mara kutoka kwa wapinzani wao Boda Boda Buza FC ambao wamekosa nafasi ya kusawazisha.
Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa TANESCO Mkoa wa Temeke, Mhandisi Ezekiel Mashola, Afisa Usalama Mwandamizi wa mkoa huo, Bw. Steven Maganga, amesema kuwa timu hiyo ilialikwa kushiriki mashindano hayo na kutumia fursa hiyo kama sehemu ya mkakati wa kuwafikia wateja, kutoa elimu kuhusu huduma za TANESCO, na kuimarisha uhusiano na jamii.
“Kupitia mashindano haya, tumeweza kuwakaribia wananchi, kuzungumza nao moja kwa moja, na kutoa elimu ya uzalendo wa kulinda miundombinu ya shirika pamoja na kuhamasisha kuwa mabalozi wa TANESCO, kwani shirika hili ni mali ya kila Mtanzania,” amesema Bw. Maganga.
Amesema kuwa kuwa michezo ina mchango mkubwa katika kuboresha afya ya wafanyakazi, jambo ambalo linaleta tija katika utendaji kazi wa kila siku.
“Mfanyakazi mwenye afya njema anaweza kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kwa muda mrefu bila kuchoka. Hii huongeza uzalishaji na ubora wa huduma zetu kwa wateja,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Kocha wa TANESCO Temeke FC ambaye pia ni Kaimu Meneja wa TANESCO Wilaya ya Yombo, Bw. Stephen Kabuzole, ameushukuru uongozi wa Mkoa kwa msaada na ushirikiano walioutoa hadi kufanikisha ushindi huo.
“Siri ya mafanikio yetu ni mshikamano wa timu, kujituma na hamasa kutoka kwa viongozi wetu. Tumeitumia fursa hii pia kuwasiliana moja kwa moja na jamii, kuelewa changamoto zao na kuwapa elimu ya matumizi sahihi kuhusu huduma zetu za umeme,” amesema Bw. Kabuzole.
Nahodha wa timu, Magesa J. Simirya, ameeleza furaha yake baada ya ushindi huo, huku akisema kuwa ushindi huo umetokana na matokeo ya mazoezi ya mara kwa mara, nidhamu na ushirikiano wa timu.
“Tumefanikisha lengo letu kwa kuwa na mshikamano, tumekuwa si timu ya mpira, bali mabalozi wa TANESCO kwa jamii,” amesema.
Fainali hizo za UVCCM Boda Boda CUP 2025 zilishirikisha jumla ya timu nane kutoka Manispaa ya Temeke, na mgeni rasmi katika hafla ya kufunga mashindano alikuwa Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Comred Yese A. Wezza, ambaye amekabidhi zawadi kwa washindi ambapo TANESCO Temeke FC wamepokea jezi seti moja na mbuzi kama zawadi ya ushindi, huku mshindi wa pili akiambulia jezi seti moja.