Na Mwandishi Wetu
Benki ya NMB imeendelea na programu yake ya NMB Kijiji Day kwa kishindo, ambapo matukio mawili makubwa yamefanyika kwa siku moja katika vijiji vya Igowole, Mafinga mkoani Iringa na Rusesa, Kasulu mkoani Kigoma, yakiambatana na utoaji wa elimu ya fedha, huduma za kifedha, elimu ya nishati safi ya kupikia, na kampeni za mazingira.
Katika kijiji cha Igowole, Mafinga, wakazi walipata fursa ya kushiriki katika warsha za elimu ya fedha kupitia mkakati maalum wa Nondo za Pesa, unaolenga kuwafikia Watanzania wengi zaidi katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma rasmi za kifedha. Elimu hiyo ilijumuisha huduma za kufungua akaunti, mikopo, bima na matumizi ya huduma za kidijitali.
Mbali na elimu ya kifedha, tukio hilo lilihusisha semina juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, mafunzo kwa vyama vya kijamii, burudani kupitia bonanza lenye michezo mbalimbali, na upandaji wa miti zaidi ya 600 kwa ajili ya kuhifadhi mazingira.
Benki iliwakilishwa na Manyilizu Masanja, Meneja wa Mauzo wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, kwa niaba ya Meneja wa Kanda.
Wakati huo huo, katika kijiji cha Rusesa, Kasulu, NMB Kijiji Day ilipamba moto kwa kuwahusisha zaidi ya vikundi 20 vya kijamii vyenye wanachama zaidi ya 600, waliopatiwa elimu juu ya huduma jumuishi za kifedha, nishati safi na utunzaji wa mazingira.
Katika tukio hilo, NMB ilikabidhi na kupanda miche 1,000 ya miti kwenye shule za msingi na sekondari za kijiji hicho, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake kwa Serikali ya Awamu ya Sita kupitia kampeni ya Milioni Moja Miti na mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Katibu Tarafa wa Buyonga Paul Ramadhan alisifu juhudi za NMB katika kuunga mkono mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na kuhimiza matumizi ya nishati safi.
“NMB wametushika mkono leo. Tumeshuhudia elimu, michezo, na kampeni za mazingira, all in one. Huu ni mfano bora wa taasisi binafsi kushiriki maendeleo ya jamii,” alisema Ramadhan.
Kwa upande wake, Meneja wa Tawi la NMB Kasulu, Ipyana Mwakatobe, alieleza kufurahishwa na mwamko wa wananchi na kuahidi kuendelea kushirikiana nao ili kukuza ustawi wa kiuchumi, kiafya na kielimu katika wilaya hiyo.
Katika bonanza lililoambatana na sherehe hizo, wakazi wa Rusesa walishiriki michezo mbalimbali ikiwemo kuvuta kamba, mpira wa miguu, mbio za baiskeli, na michezo ya jadi kama bao na drafti. Mechi ya fainali ya mpira wa miguu iliwashuhudia wenyeji Rusesa City FC wakiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya New Generation Academy ya Kasulu.
NMB inatarajia kufikia zaidi ya vijiji 2,000 kupitia Kijiji Day mwaka huu, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia Watanzania wote, hata walioko vijijini.