Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Profesa Adolf Mkenda (katikati) akikata utepe wakati akizundua magari maalum ya kubeba watoto wachanga (Ambulensi) kwa ajili ya huduma za dharura katika hafla fupi iliyofanyika hivi karibuni Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Kampasi ya Mloganzila, Dar es Salaam. (PICHA NA NOEL RUKANUGA)
Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Afya, Idara ya Afya ya Mtoto na Vijana, Dkt. Felix Bundala akizungumza na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa mradi maalum uitwao Breath for Babies (BfB), wenye lengo la kupunguza vifo vya watoto wachanga wenye umri wa siku 0 hadi 28 katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mtafiti Mkuu Msaidizi wa mradi maalum uitwao Breath for Babies (BfB), ambaye pia ni Daktari Bingwa wa watoto wachanga kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) Dkt. Martha Mkony, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa mradi huo wenye lengo la kupunguza vifo vya watoto wachanga wenye umri wa siku 0 hadi 28 katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Amana, Dkt. Bryson Kiwelo akizungumza na waandishi wa habari kuhusu umuhimu wa mradi maalum uitwao Breath for Babies (BfB), wenye lengo la kupunguza vifo vya watoto wachanga wenye umri wa siku 0 hadi 28 katika Mkoa wa Dar es Salaam.
……….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Ifakara Health Institute kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) pamoja na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wamezindua rasmi mradi maalum uitwao Breath for Babies (BfB), wenye lengo la kupunguza vifo vya watoto wachanga wenye umri wa siku 0 hadi 28 kutoka vifo 24 hadi 12 kwa kila watoto 1,000 waliozaliwa ifikapo mwaka 2030.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika jijini Dar es Salaam, wakati wa kupokea magari maalum ya kubeba watoto wachanga (ambulensi) kwa ajili ya huduma za dharura, Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Afya, Idara ya Afya ya Mtoto na Vijana, Dkt. Felix Bundala amesema kuwa huduma hizo zitasimamiwa na MUHAS kwa ajili ya kusaidia watoto wachanga katika Mkoa wa Dar es Salaam, hususan wale wenye matatizo ya kupumua, uzito pungufu, na magonjwa ya kuambukiza.
“Mradi huu mpya unalenga kuwasaidia watoto wachanga tangu wanapozaliwa, hasa wale wenye changamoto za upumuaji. MUHAS inatekeleza kwa vitendo maono ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuhakikisha huduma za watoto wachanga zinaboreshwa na vifo vinapungua,” amesema Dkt. Bundala.
Dkt. Bundala ameongeza kuwa Serikali imeongeza idadi ya wodi za watoto wachanga kutoka 14 mwaka 2018 hadi kufikia 318 mwaka 2025. Aidha, kuna mikakati ya kuimarisha miundombinu, ununuzi wa vifaa tiba, na kuongeza idadi ya watoa huduma wenye ujuzi.
Amesema kuwa programu hiyo imeanza kutekelezwa katika Mkoa wa Dar es Salaam kutokana na ukubwa wa changamoto, ambapo watoto wapatao 12,500 huzaliwa kila mwezi na kati yao, takribani 2,500 huhitaji huduma maalum.
Dkt. Bundala ametoa wito kwa akina mama wajawazito kuhudhuria kliniki na kujifungua katika vituo vya afya ili kujikinga na hatari zinazoweza kuepukika, huku akibainisha kuwa asilimia 20 ya wajawazito bado hujifungulia nyumbani.
Amesema kuwa serikali imeongeza idadi ya vituo vya dharura kwa wajawazito kutoka 115 mwaka 2015 hadi 549 kufikia sasa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha huduma za uzazi.
Kwa upande wake, Mtafiti Mkuu Msaidizi wa mradi huo, ambaye pia ni Daktari Bingwa wa watoto wachanga kutoka MNH, Dkt. Martha Mkony, amesema kuwa mradi huo unafadhiliwa na Bill & Melinda Gates Foundation na unatekelezwa na watafiti kutoka MUHAS, MNH na Ifakara Health Institute kwa lengo la kufikia malengo yaliyowekwa.
“Mradi huu unalenga kutoa huduma stahiki kwa watoto wachanga tangu wanapozaliwa, kuwapatia tiba ya haraka ya upumuaji, na kutoa mafunzo kwa watoa huduma hospitalini na wale wanaofanya kazi katika ambulensi za watoto,” amesema Dkt. Mkony.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Amana, Dkt. Bryson Kiwelo, amesema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vya watoto na wajawazito kwa muda mfupi.
Amebainisha kuwa vifo vya wajawazito vinavyotokana na uzazi vimepungua kutoka 556 hadi wastani wa 104 kwa kila vizazi hai 100,000.
Dkt. Kiwelo ameongeza kuwa taasisi nyingine kama Ifakara Health Institute na NEST360 zimeungana katika juhudi hizo kwa kutengeneza mifumo ya kusaidia watoto wachanga kupumua vizuri.