Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Mkurugezi Mtendaji wa kituo Cha Ubia Sekta binafsi na Sekta ya umma (PPPs) na mtaalamu wa sera za maendeleo, David Kafulila, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mjadala wa kihistoria kuhusu nafasi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPs) unaotarajiwa kufanyika kesho katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Mjadala huu una lengo mahsusi la kuchambua na kutoa mapendekezo kuhusu mchango wa PPPs katika kufanikisha Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.
Mjadala huo unaratibiwa na Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC) kwa kushirikiana na Kituo cha Utafiti wa Demokrasia na Utawala Bora (REDET) cha UDSM. Kwa pamoja, taasisi hizo zinalenga kuibua mjadala mpana kuhusu namna ubia huo unavyoweza kuchochea uchumi jumuishi na endelevu katika muktadha wa dira mpya ya taifa.
Katika mdahalo huo, viongozi na wataalamu mbalimbali wa sekta tofauti wanatarajiwa kushiriki, akiwemo Profesa Rwekaza Mukandala, Waziri wa zamani wa Ardhi Profesa Anna Tibaijuka, na David Kafulila mwenyewe ambaye atatoa mada kuu kuhusu maandalizi ya ubia katika sekta ya uchumi kuelekea mwaka 2050.
Kafulila amesisitiza kuwa mjadala huo ni wa kihistoria kwa kuwa unalenga kutoa mwelekeo wa kitaifa kuhusu nafasi ya sekta binafsi katika kusaidia maendeleo ya nchi. Alieleza kuwa dira ya 2050 inahitaji ushirikiano imara kati ya serikali na sekta binafsi ili kufanikisha malengo ya kitaifa ya kiuchumi, kielimu, na kijamii.
“Kupitia mjadala huu, tunataka kuweka msingi wa ushirikiano imara baina ya sekta ya umma na binafsi, kwa ajili ya kuharakisha maendeleo ya taifa letu. Wananchi washiriki kwa wingi kutoa mawazo yao,” alisema Kafulila wakati wa mahojiano na waandishi wa habari.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Mpango wa utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET) Rwekeza Mkandara Ameeleza kuwa mjadala huu unatoa fursa ya kipekee kwa Watanzania kutoka sekta mbalimbali kuchangia maoni yao kuhusu mustakabali wa taifa letu.
, Profesa Mukandala, aliendelea kusema kuwa ushirikiano huu ni mfano bora wa demokrasia ya kweli na ushirikishwaji wa wananchi katika kupanga maendeleo yao.
Mjadala huu unakuja wakati taifa likielekea kuandaa dira mpya ya maendeleo, na hivyo kutoa fursa kwa wadau wote kujadili kwa kina ni vipi Tanzania inaweza kufikia uchumi wa kati wa juu na hatimaye wa viwanda kupitia ubia wenye tija kati ya sekta ya umma na binafsi.