Na Mwamvua Mwinyi
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini na Msemaji Mkuu wa Wizara ya TAMISEMI, John Mapepele, ametoa rai kwa maofisa Habari wa Mikoa na Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanatanguliza uzalendo na weledi katika utoaji wa taarifa, ili habari wanazozitoa ziwe na manufaa kwa taifa.
Mapepele alitoa wito huo mwishoni mwa wiki alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu Mawasiliano ya Kimkakati ya Kutangaza Mafanikio ya Sekta za Afya, Elimu na Miundombinu chini ya TAMISEMI kwa Maafisa Habari zaidi ya 200 kutoka mikoa na halmashauri mbalimbali nchini.
Mafunzo hayo yalifanyika jijini Dodoma katika kikao kazi cha siku mbili kilichoratibiwa na wizara hiyo.
Kikao kazi hicho kilifunguliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais–TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, na kufungwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa.
Pamoja na kujadili mikakati ya kutangaza mafanikio ya Serikali, kikao hicho kililenga kuwajengea uwezo Maofisa Habari kwa mada mbalimbali za kitaaluma, hasa matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa taarifa, na kutoa maazimio ya kuboresha utendaji kazi.
Mapepele alisema, kumekuwa na mafanikio makubwa katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika mikoa na halmashauri mbalimbali nchini, lakini taarifa zake hazijatangazwa ipasavyo. Hivyo, aliwataka Maafisa Habari kuwa wabunifu na makini katika kuibua na kuwasilisha taarifa hizo kwa wananchi.
“Ndugu zangu, Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya mapinduzi makubwa katika sekta ya miundombinu. Tumeona barabara, madaraja, vituo vya mabasi na masoko vikijengwa kila uchao.
Vilevile, madarasa, zahanati, vituo vya afya na vifaa tiba vimeboreshwa katika kila kona ya nchi. Ni wajibu wetu sisi Maafisa Habari wa Halmashauri na Mikoa kuwa wazalendo kwa kuisemea Serikali yetu ili wananchi wajue na kutumia huduma hizi kikamilifu,” alieleza Mapepele.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi hicho, Mchengerwa aliwataka Maafisa Habari wa TAMISEMI kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao.
“Mmebeba dhamana kubwa ya kuhakikisha wananchi wanapata habari sahihi,Msikubali Watanzania walishwe habari potofu,” alisisitiza Mchengerwa.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Gerson Msigwa aliupongeza uongozi wa TAMISEMI kwa kuratibu kikao kazi hicho na kushauri kiwe kinazungumziwa kuwa cha kila mwaka ili kufanya tathmini ya kazi na kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili Maafisa Habari katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mara baada ya kikao hicho, Maafisa Habari walipata fursa ya kutembelea Mji wa Serikali wa Mtumba na kujionea maendeleo ya ukamilishaji wa miundombinu ya mji huo.


