Na John Bukuku Dar es Salaam
Aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki, amesema kuwa ujenzi wa viongozi wenye uwezo wa kusimamia na kutekeleza sera ndio njia bora ya kuleta maendeleo endelevu barani Afrika.
Akizungumza katika Mhadhara wa Siku ya Afrika uliofanyika leo jijini Dar es Salaam, Mbeki alieleza kuwa Afrika imejaa maono mazuri na sera bora, lakini changamoto kubwa ni utekelezaji unaotokana na mapungufu katika uongozi wa kisera na kiutendaji.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Mbeki alisema aliunda Taasisi ya Uongozi wa Afrika kupitia Chuo Kikuu cha Afrika Kusini (UNISA), baada ya ushauri kutoka kwa wenzake waliotaka aendelee kuchangia maendeleo ya bara hata baada ya kustaafu urais mwaka 2008.
“Tuliona umuhimu wa kuwa na taasisi itakayowajengea uwezo viongozi wa Afrika. UNISA ilichaguliwa kwa sababu ni taasisi ya masafa inayofikia zaidi ya nchi 40 barani Afrika,” alisema Mbeki.
Akitambua umuhimu wa kushirikisha bara zima katika mijadala ya maendeleo, Mbeki alisema mihadhara ya Siku ya Afrika imekusudiwa kufanyika katika nchi mbalimbali ili kufikia viongozi, wasomi na wananchi wengi zaidi. Alisisitiza kuwa “hii ni taasisi ya Kiafrika, si ya taifa moja.”
Tanzania imekuwa mwenyeji wa mhadhara huo kwa mara ya tatu, jambo ambalo Mbeki alisema ni ishara ya kujitolea kwa Taifa hilo katika kukuza fikra za maendeleo na mshikamano wa Kiafrika. Aliwataja viongozi wengine waliowahi kutoa mihadhara hiyo kuwa ni pamoja na Hayati Rais Benjamin Mkapa na Salim Ahmed Salim.
Katika hotuba yake, Mbeki aliwahimiza viongozi na wananchi wa Afrika kuchukua hatua za vitendo katika kutekeleza sera na maono yaliyoanzishwa kwa maendeleo ya bara. “Uamsho wa Afrika (African Renaissance) unahitaji zaidi ya ndoto; unahitaji elimu, uongozi mahiri na utekelezaji wa kweli,” alisisitiza.