Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mara kimeiagiza serikali mkoani humo kujenga sanamu ya Mwalimu Julius Nyerere katika makutano ya barabara ya Mwanza – Musoma yaliyopo eneo la Ziroziro wilayani Butiama ili pamoja na mambo mengine liweze kutumika kama kama alama ya utambulisho wa mkoa.
Pia chama hicho kimeiagiza serikali mkoani huno kuhakikisha inajenga mizunguko yote (roundabouts ) zilizopo ndani ya kila wilaya na kuwa za kisasa ziaid tofauti na ilivyo sasa ambapo mizungunguko hiyo imeachwa bila kujengwa hali ambayo inatoa taswira mbaya.
Maagizo hayo yametolewa leo Mei 23 2025 mjini Musoma katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa
Mara kilichoketi kwaajili ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya 2020/25 kwa mkoa huo.
Katibu wa CCM Mkoa wa Mara, Iddi Mkowa amesema maagizo hayo yanatokana na maazimio yaliyofanywa na kamati kuu ya siasa ya mkoa baada ya kufanya ziara katika maeneo mbalimbali ndani ya mkoa huo ambapo pamoja na mambo mengine waliona ipo haja ya serikali kufanyia kazi maagizo hayo.
“Ijengwe sanamu nzuri na ya kisasa ya baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere pale Ziroziro kwasababu tumebaini licha ya kuwa Mwalimu Nyerere anatokea mkoani Mara lakini hakuna sehemu yoyote ambayo kuna sanamu yake ndani ya mkoa tofauti na mikoa mingine lakini pia tumebaini mkoa wetu hauna alama maalum ya utambulisho kama ilivyo mikoa mingine,” amesema
Amesema katika mzunguko uliopo ndani ya Manispaa ya Musoma serikali inatakiwa kujenga na kuweka luninga ambayo itakuwa ikionyesha vivutio vya uwekezaji na uchumi ikiwepo utalii vilivyopo ndani ya mkoa sambamba na miradi ambayo imetekelezwa na ile inayoendelea kutekelezwa ndani ya mkoa.
Kuhusu utekelezaji wa miradi, chama hicho kimempongeza Mkuu wa Mkoa huo kwa namna ambavyo ameweza kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo na kwamba utekelezaji huo unezingatia thamani halisi ya fedha.
“Jana na juzi kamati ya siasa imetembelea miradi 38 katika wilaya zote,tumeridhishwa na utekelezaji wa miradi ile tunakupongeza mkuu wa mkoa kwa namna ulivyowezava kusimamia utekelezaji wa miradi endelea hivyo hivyo kwani miradi hiyo lengo lake ni kuwanufaisha wananchi,” amesema
Akizungumza kuhusu maagizo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amesema tayari ofisi yake ilikwishatoa maelekezo kwa wakuu wa wilaya za Butiama na Musoma pamoja na wakurugenzi wa halmashauri hizo kuanza mchakato wa ujenzi wa mizunguko hiyo.
“Nikuhakikishie kuwa uhitaji wa uwepo wa sanamu ya Mwalimu Nyerere na mzunguko mzuri wenye kupendeza katika mji wetu tayari tulishaona upo uhitaji huo na kuwaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi wao kufanyia kazi,mchakato tayari umeanza na kutokana na maagizo haya tunakwenda kuongeza kasi,” amesema Kanali Mtambi
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM mkoani Mara, Kanali Mtambi amesema serikali imetumia mabilioni ya shilingi kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta tofauti miradi ambayo imeleta tija kwa wanachi kwani imesaidia kuboresha huduma mbalimbali za kijamii.
Ametolea mfano wa zaidi ya Sh2.93 bilioni zilizotolewa na mamlaka za serikali za mitaa mkoani humo kwaajili ya mikopo isiyokuwa na riba kwa makundi ya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu kwa mwaka 2024 hadi Februari mwaka huu.
Amesema mikopo hiyo imenufaisha vikundi 324 kutoka katika halmashauri tisa za mkoa huo ambapo kati ya hivyo vikundi 86 vilikuwa ni vya watu wenye ulemavu.
Kuhusu sekta ya miundombinu, Kanali Mtambi amesema serikali imetoa zaidi ya Sh240 bilioni kati ya mwaka 2020 hadi 2024 kwaajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu ikiwepo ujenzi wa uwanja wa ndege wa Musoma, mzani unaopima magari yakiwa kwenye mwendo pamoja na barabara kadhaa kwa kiwango cha lami.
“Miradi 38 mliyopata fursa ya kutembelea jana na juzi ni sehemu ndogo sana ya miradi iliyotekelezwa mkoani kwetu, serikali imegusa sekta zote ikiwepo maji,miundombinu, afya, elimu,uvuvi madini na zinginezo ipo miradi iliyokamilika na mingine ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na hii inamaana huduma zimeboreshwa kwa kiwango kikubwa,” amesema Mtambi
Amesema pamoja na mafanikio hayo zipo changamoto kadhaa zilizobainika katika kipindi hicho cha utekelezaji wa ilani ikiwepo suala la upungufu wa watumishi pamoja na vitendo vya uvamizi ndani ya ziwa Victoria vinavyofanywa na watu kutoka nchi jirani.
Kuhusu changamoto hiyo ya wavuvi kuvamiwa ndani ya ziwani,Kanali Mtambi amesema zipo hatua kadhaa zimechukuliwa ili kudhibiti hali hiyo ikiwa ni pamoja na kuhusisha jeshi la wananchi kwa kitengo cha wana maji kufanya doria maalum ndani ya ziwa hilo ili wavuvi wa Tanzania waweze kufanya shughuli zao kwa usalama.
Baadhi ya wakazi wa Musoma wameiomba serikali kuhakikisha kuwa wavuvi wa Tanzania wanakuwa salama muda wote wanapofanya shughuli zao kwa maelezo kuwa vitendo vya uvamizi vinazidi kuongezeka.
“Mimi ni mvuvi na hawa watu wanatusumbua sana,tunanyang’anywa zana zetu na samaki pia, hii ni hasara kubwa unatumia rasiliamli fedha na muda mwisho wa siku wanakuja watu na silaha za moto wanakunyang’anya,huu mpango wa kutumia jeshi la wananchi nadhani unafaa sana,” amesema Philipo Magebo