Shirika la TradeMark Africa (TMA) limechangia kwa kiasi kikubwa mageuzi ya kidijitali ndani ya Tume ya Ushindani (FCC) kwa kutoa msaada wa dola 600,000, ikiwa ni sehemu ya dhamira yake ya kuimarisha taasisi za biashara barani Afrika kupitia ubunifu wa kiteknolojia.
Kupitia ufadhili huo, FCC imepiga hatua muhimu kwa kumpokea rasmi mkandarasi wa ndani — kampuni ya ICTPACK — atakayetekeleza mradi wa otomatiki wa shughuli za ndani za taasisi hiyo. Mradi huo unalenga kuiwezesha FCC kubadilisha mifumo yake ya sasa na kuwa ya kisasa, yenye kujibu kwa haraka na kwa ufanisi mkubwa.
Akizungumza katika kikao cha kimkakati kilichofanyika jijini Dar es Salaam Mei 22, 2025, mwakilishi wa Mkurugenzi wa Nchi wa TMA Erick, Bi. Lilian Masalu, alisema kuwa shirika hilo linatilia mkazo matumizi ya TEHAMA kama njia ya kurahisisha biashara na kuongeza ushindani wa kiuchumi.
“Lengo letu ni kufanya biashara iwe rahisi. Tunaamini taasisi kama FCC zikifanya kazi kidijitali, zitaharakisha maamuzi na kuongeza uwazi,” alisema Bi. Masalu. “Tulianza kwa kufanya utafiti wa kina, tukachagua mkandarasi kupitia ushindani, na sasa tupo tayari kusaidia kwa karibu utekelezaji wake.”
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa FCC, William Erio, licha ya mkataba rasmi wa utekelezaji kuwa bado haujasainiwa, zaidi ya asilimia 75 ya maandalizi ya awali ya mradi yameshakamilika. Alieleza kuwa nia ya FCC ni kuhakikisha kuwa mfumo huo mpya unazinduliwa mapema iwezekanavyo.
“Mabadiliko ya kiteknolojia yanakwenda kwa kasi. Tusipobadilika sasa, tutapitwa. Huu ni mradi muhimu kwa ustawi wetu kama taasisi ya kisheria,” alisema Erio huku akiahidi ushirikiano wa karibu na ICTPACK kuhakikisha mradi huo unaenda kwa kasi bila kupoteza ubora.
Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa kwa miaka miwili; mwaka wa kwanza ukiwa wa kuunda mifumo na mwaka wa pili kwa mafunzo na uhamishaji wa maarifa kwa watumishi wa FCC.
Kwa upande wake, Meneja Mradi wa ICTPACK, Bw. Renatus Ng’homi, aliwasilisha taarifa ya mwanzo ya mradi ikionyesha hatua, matumizi ya rasilimali na utaratibu wa usimamizi wa utekelezaji.
Bi. Masalu alisisitiza kuwa TMA imeunda timu maalum itakayoshirikiana na idara ya TEHAMA ya FCC katika kila hatua ya mradi, ili kuhakikisha kuna usimamizi wa pamoja na mafunzo endelevu.
“Mradi huu hauhusu teknolojia tu. Unahusu kujenga taasisi thabiti, inayoaminika, inayoweka mazingira bora ya ushindani wa haki,” alisema.
Kwa msaada huu wa TMA, serikali imeepushwa mzigo wa kifedha wa kuendesha mradi huu, huku rasilimali za umma zikielekezwa katika maeneo mengine ya kipaumbele cha taifa.
FCC sasa iko tayari kuanza safari yake mpya ya kidijitali — hatua inayoiweka mstari wa mbele katika mageuzi ya sekta ya umma na kuimarisha ushindani wa kiuchumi nchini Tanzania.