Dar es Salaam, Mei 20, 2025.
Tanzania na Namibia zimeanza ukurasa mpya wa ushirikiano wa kimkakati unaolenga kuinua uchumi wa mataifa hayo kupitia sekta za nishati, biashara, uwekezaji na uchumi wa buluu. Hayo yameelezwa leo jijini Dar es Salaam na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, mara baada ya kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Namibia, Netumbo Nandi-Ndaitwah, aliye katika ziara rasmi nchini.
Rais Dk. Samia amesema mazungumzo yao yamejikita zaidi katika kuongeza ushirikiano wa kiuchumi, hasa kwa kuzingatia kuwa bado kuna nafasi kubwa ya kushirikiana kibiashara licha ya ongezeko la thamani ya biashara baina ya nchi hizo kutoka shilingi bilioni 17 mwaka 2019 hadi bilioni 20 mwaka 2023.
“Tumeona bado kuna pengo kubwa la kushirikiana kibiashara na kimitaji, na kwa pamoja tumekubaliana kulijazia pengo hilo kwa hatua za pamoja,” amesema Dk. Samia.
Katika hatua ya kukuza fursa hizo, Rais Dk. Samia amewaomba wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Namibia kushiriki Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF) mwaka huu, kama jukwaa la kubadilishana uzoefu na kujifunza fursa zilizopo nchini.
Aidha, wakuu hao wa nchi wamezielekeza wizara husika kuandaa mikutano ya mara kwa mara ya wafanyabiashara na wawekezaji wa pande zote mbili, kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kukuza mitaji ya uwekezaji.
Katika eneo la nishati, nchi hizo mbili zimekubaliana kushirikiana katika uchakataji wa mafuta na gesi, hatua ambayo inalenga kuhakikisha rasilimali hizo zinawanufaisha wananchi.
Kwa upande wake, Rais Netumbo Nandi-Ndaitwah wa Namibia amesema kuwa nchi yake imefungua milango kwa ushirikiano na Tanzania katika sekta ya nishati, hasa ikizingatiwa kuwa Namibia ni nchi ya tatu duniani kwa utajiri wa madini ya urani.
Rais huyo pia ameweka wazi nia ya Namibia kushirikiana na Tanzania katika kukuza uchumi wa buluu kwa kubadilishana uzoefu na maarifa kutokana na mafanikio ambayo nchi yake imeyapata katika kutumia rasilimali za baharini.