Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo amempokea Rais wa Jamhuri ya Finland, Mhe. Alexander Stubb, ambaye yuko nchini kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Finland.
Taarifa iliyotolewa na Shaaban Kissu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu imesema Marais hao wawili walifanya mazungumzo ya faragha, kisha kuongoza mazungumzo rasmi kati ya ujumbe wa Tanzania na ule wa Finland, yaliyolenga kuimarisha na kupanua wigo wa ushirikiano wa kidiplomasia na kimaendeleo kati ya mataifa hayo mawili, ambao mwaka huu unatimiza miaka 60 ya uhusiano.
Rais Dkt. Samia alieleza kuwa mazungumzo hayo yamegusia maeneo mbalimbali yanmaendeleo ikiwemo misitu, biashara, uwekezaji, madini, elimu, utalii, uwezeshaji wa
wanawake, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), nishati safi ya kupikia pamoja na uchumi wa buluu. Alibainisha pia kuwa Tanzania na Finland zimeonesha utayari wa kutumia fursa zilizopo katika maeneo hayo kwa manufaa ya pande zote mbili.
Aidha, Rais Stubb anatarajiwa kuzindua rasmi mpango wa Maendeleo ya Misitu, Matumizi ya Ardhi na Minyororo ya Thamani nchini Tanzania (Forestry, Land Use, and Value Chains Development in Tanzania – FORLAND), unaolenga kuzijengea uwezo taasisi za elimu ya misitu nchini.
Kwa upande mwingine, Tanzania imetoa wito kwa Finland kushirikiana katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia, unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ifikapo mwaka 2034.
Katika sekta ya elimu, Tanzania imeishukuru Finland kwa mchango wake mkubwa katika kukuza elimu ya ufundi stadi, mafunzo ya kidijitali na kuwajengea uwezo walimu.
Marais hao pia walikubaliana kuendeleza ushirikiano wa kitaasisi kupitia Taasisi ya UONGOZI Institute inayolenga kukuza uongozi bora, hususan kwa wanawake.
Sekta ya madini nayo imepewa kipaumbele ambapo Tanzania imeikaribisha sekta binafsi
ya Finland kuwekeza katika maeneo ya uongezaji thamani madini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza uchumi wa ndani na kuongeza ajira kwa vijana.
Rais Dkt. Samia pia alipongeza hatua ya Rais Stubb kuambatana na ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Finland, hatua inayoonesha dhamira ya kuimarisha mahusiano ya
kiuchumi kati ya nchi hizi mbili.
Katika masuala ya kimataifa, Tanzania na Finland zimekubaliana kuendeleza ushirikiano ndani ya Umoja wa Mataifa na majukwaa mengine ya kimataifa katika kushughulikia
changamoto za dunia zikiwemo amani, afya, mazingira na maendeleo endelevu.
Kwa upande wake, Rais Alexander Stubb alieleza kuwa ziara yake nchini Tanzania ni uthibitisho wa dhamira ya Finland kuendeleza na kupanua uhusiano wa muda mrefu kati
ya mataifa hayo mawili.
Kadhalika, alitambua mchango wa kihistoria wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa Afrika, hususan kupitia ushirikiano na Rais Mstaafu wa Finland, Hayati Martti Ahtisaari,
katika juhudi za upatanishi na maendeleo barani Afrika.
Rais Stubb pia alitambua nafasi muhimu ya Tanzania katika kukuza ushawishi wa bara la Afrika kwenye majukwaa ya kimataifa na akasisitiza haja ya marekebisho ya mfumo wa
kimataifa wa kufanya maamuzi ili kuakisi hali halisi ya dunia ya sasa.
Rais Stubb atahitimisha ziara yake tarehe 16 Mei, 2025 ambapo ataagwa rasmi na mwenyeji wake Rais Dkt. Samia Ikulu Jijini Dar es Salaam.