Mkurugenzi wa usambazaji wa maji manispaa ya Sumbawanga wakati akizungumza na waandishi wa habari
…………..
Na Neema Mtuka , Sumbawanga
Rukwa: Zaidi ya wakazi 15,000 wameunganishwa na huduma ya maji safi na salama katika Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi.
Akizungumza na waandishi wahabari leo Mei 14 ,2025 Mkurugenzi wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Sumbawanga (SUWASA), Ndugu Maunda Cyprian Mbenero, amesema mahitaji ya maji kwa Manispaa ya Sumbawanga kwa siku ni lita milioni 29, lakini uwezo wa sasa wa uzalishaji wa maji ni lita 230,000 pekee.
Ameeleza kuwa ili kukabiliana na changamoto hiyo, serikali imepanga kujenga bwawa kubwa katika Msitu wa Mbizi litakalokuwa na uwezo wa kuhifadhi lita milioni saba za maji. Mradi huo unatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni moja.
Mbenero pia alifichua kuwa zaidi ya kesi 23 za wizi wa mita za maji zimeripotiwa na wananchi katika maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo, na mamlaka inaendelea kushughulikia tatizo hilo kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama
“Kuna baadhi ya wananchi ambao sio wazalendo wanadiliki kuharibu miundombinu ya maji kwa kuiba mita za maji na kuuza tunasema hatutavumilia vitendo hivyo hatua Kali zitachukuliwa kwa yeyote atakaye bainika amefanya kosa hilo” amesema Mbenero
Amewasisitiza wananchi kuhakikisha wanatumia maji safi na salama na kuacha kutumia maji ya madimbwi na visima vifupi ili kujiepusha na magonjwa yatokanayo na unywaji wa maji yasiyo salama.
Amesema baadhi ya wananchi wamechimba visima karibu na choo mita 10 jambo hilo linahatarisha usalama wa afya zao kwa kuwa ni rahisi kupata magonjwa ya kuhara na tumbo.
Miongoni mwa wahanga wa wizi wa mita za maji Edison mlwela kwa masikitiko makubwa amesema kuwa yeye aliibiwa mita na hivyo alikosa huduma ya maji na kusababisha hasara kwa mamlaka ya maji.
“Baada ya changamoto hiyo niliingia gharama ya kununua mita nyingine jambo ambalo linarudisha nyuma maendeleo naiomba mamlaka husika kuhakikisha inatoa elimu kwa wananchi”.amesem mlwela.
Mlwela ameiomba Serikali pamoja na mamlaka husika kuhakikisha sheria zilizowekwa zinasimamiwa ipasavyo ili kuwalinda wananchi wanaozingatia taratibu.
Pia ameeleza umuhimu wa ushirikiano kati ya Jamii katika kuzuia uhalifu huo unaohujumu jitihada zaserikali za kuboresha maisha ya wananchi.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kutunza miundombinu ya maji pamoja na kutoa taarifa kwa mamlaka pindi wanapobaini vitendo vya kihalifu vinavyohujumu huduma hiyo muhimu.