Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Ronald Lamola (Mb) amewasili nchini kwa ziara ya kikazi.
Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Mhe. Lamola alilakiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania Afrika Kusini Mhe. James Bwana na Balozi wa Afrika Kusini nchini Mhe. Noluthando Mayende-Malepe na maafisa waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Akiwa nchini, Mhe. Lamola anatarajiwa kuwa na mazungumzo na mwenyeji wake, mazungumzo ambayo yanalenga kujadili maeneo yenye maslahi ya pamoja.
Vilevile, mawaziri hao wanatarajiwa kuangalia na kutafuta fursa mpya za ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.
Ziara hii inalenga kuendelea kuimarisha uhusiano wa uwili kati ya Tanzania na Afrika Kusini na kukuza ushirikiano wa kimkakati katika maeneo mbalimbali ya maendeleo.
Ziara hii pia ni ishara ya mafanikio katika uhusiano wa kihistoria na kindugu uliopo kati ya mataifa haya mawili, ambao ulijengwa juu ya misingi ya pamoja, na mshikamano wa muda mrefu, hususan kutokana na mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa Afrika Kusini.