Wafugaji wa ng’ombe wa maziwa jijini Tanga wamenufaika na mafunzo ya homa ya kiwele (mastitis) yanayotolewa kupitia mradi wa NANO COM unaoendeshwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ambao unafadhiliwa na Kituo cha Kimataifa cha Maendeleo ya Utafiti cha Canada (IDRC).
Akizungumza wakati wa mafunzo yaliyofanyika jijini humo, mtafiti kiongozi wa mradi huo, Prof. Gaymary Bakari amesema kuwa, lengo la mafunzo hayo ni kutoa mrejesho kwa wafugaji na kutambua changamoto wanazokumbana nazo.
“Mafunzo haya ni sehemu ya tathmini ya hali halisi ya homa ya kiwele katika mkoa wa Tanga, baada ya kufanya utafiti wa awali, sasa tumeleta mrejesho na kuwasikiliza wafugaji ili kuelewa changamoto na namna ya kuimarisha tiba tunayoendelea kuibuni,” alisema Prof. Bakari.
Kwa upande wake, Dkt. Rashid Chonga Nasoro, Afisa Mifugo kutoka Halmashauri ya Jiji la Tanga, aliipongeza SUA kwa kupeleka elimu hiyo kwa wafugaji.
“Mafunzo haya yatasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza athari za homa ya kiwele. Tumejifunza njia sahihi za kukinga na kudhibiti ugonjwa huu,” alisema Dkt. Chonga.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wafugaji waliohudhuria mafunzo hayo walieleza namna elimu hiyo ilivyowaongezea uelewa. Winnie Lema kutoka Kata ya Mzizima alisema mafunzo hayo yamemsaidia kufahamu umuhimu wa usafi wakati wa kukamua ng’ombe, huku Hamza Mshana wa Kata ya Kiomoni akieleza kuwa wamejifunza makosa ambayo awali walikuwa wakiyafanya bila kujua.
Mradi wa NANO COM unatekelezwa katika mikoa mitano nchini ambayo ni Tanga, Iringa, Mbeya, Njombe na Arusha. Tafiti katika maeneo haya zinalenga kubaini vyanzo vya homa ya kiwele na kubuni tiba mbadala kwa ajili ya wafugaji nchini Tanzania.